UONGOZI wa Singida Black Stars umekamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji, Mossi Nduwumwe, baada ya mabosi wa kikosi hicho kuvutiwa na uwezo wa mchezaji huyo anayeichezea Flambeau du Centre FC ya kwao Burundi.
Singida ilikuwa inapambana kukamilisha usajili wa nyota huyo anayecheza winga ya kulia na kushoto, huku pia akitokea nyuma ya mshambuliaji ikidaiwa huenda ni mbadala wa kiungo mshambuliaji, Idriss Diomande anayeweza kutua Azam.
Diomande aliyejiunga na Singida Agosti 20, 2025, akitokea Zoman FC ya kwao Ivory Coast, huenda akajiunga na Azam baada ya mabosi wa timu hiyo kuanza kufuatilia saini yake, wakipambana kumpata kabla ya usajili haujafungwa Januari 30, 2026.
Nduwumwe aliyezaliwa Januari 1, 2002, alijiunga na Flambeau du Centre FC Julai 1, 2023, baada ya kuachana na Musongati FC ya kwao pia Burundi, ambapo aliwavutia zaidi mabosi wa Singida walipokutana katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Singida ilikutana na Flambeau katika hatua ya pili kusaka tiketi ya kufuzu makundi, ambapo ilifuzu kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare ya bao 1-1, Burundi, Oktoba 19, 2025, kisha kushinda jijini Dar es Salaam mabao 3-1, Oktoba 25, 2025.
Mwanaspoti linatambua Singida imeanza mchakato wa kuhakikisha inampata Nduwumwe ili awe mbadala wa Diomande ikiwa nyota huyo ataondoka, ikiwa ni muda mfupi baada ya kumsajili, Linda Mtange aliyetokea FC Les Aigles du Congo ya kwao DR Congo.
Mtange anayecheza kiungo mshambuliaji, ameichezea pia Hearts of Oak ya Ghana, ambapo nyota huyo aliyezaliwa Novemba 26, 2022, amejiunga na kikosi hicho kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Clatous Chota Chama ‘Triple C’, aliyerejea tena Simba.