Mgosi ataja jeuri ya Simba Queens

KOCHA wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi’, amesema ushindi dhidi ya Alliance Girls katika Ligi Kuu Soka Wanawake, ni matokeo ya maandalizi mazuri na nidhamu ya hali ya juu kutoka kwa wachezaji wake.

Juzi, Simba Queens ilipata ushindi wa bao 1-0 mbele ya Alliance Girls katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza na kutibua rekodi ya wenyeji kucheza mechi tisa za ligi kwenye uwanja huo bila kupoteza.

Matokeo hayo yanaifanya Simba Queens iendelee kukaa kileleni kwa alama 28 katika mechi 10, ikifuatiwa na Yanga Princess iliyo na alama 24, huku Alliance Girls ikibaki nafasi ya nne na alama zake 19.

“Tulijipanga kupata ushindi tangu mwanzo na tunamshukuru Mungu tumefanikiwa kushinda mchezo wetu. Alliance Girls walicheza mpira mzuri na walituweka kwenye presha, lakini walifanya kosa moja ambalo tulilitumia vizuri kuwaadhibu,” alisema Mgosi.

Kocha huyo alieleza kuwa falsafa ya Simba Queens msimu huu ni kuhakikisha wanapambana kila mchezo kwa lengo la kupata alama tatu bila kubeza mpinzani yeyote, akisisitiza kuwa mafanikio yao yanatokana na umoja na kujituma kwa kikosi kizima.

“Nawapongeza sana wachezaji wangu kwa kujituma, nidhamu na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi. Kila mechi tunajiandaa kwa malengo yale yale ya kushinda na kukusanya alama tatu,” aliongeza.

Kwa upande wa Alliance Girls, Kocha Mkuu, Sultan Juma alisema timu yake ilijitahidi kupambana lakini ilikumbwa na changamoto ya kukosa umakini hasa katika kipindi cha mwisho cha mchezo, hali iliyowagharimu kupoteza ushindi au angalau kupata pointi.

“Tulicheza vizuri kwa sehemu kubwa ya mchezo, lakini tulikosa umakini katika dakika za mwisho na wenzetu walitufunga kwa kutumia faulo. Pia tulifanya makosa katika kupanga ukuta wa kujilinda, jambo lililotuumiza,” alisema Sultan.

Alisema uchovu uliwaathiri baadhi ya wachezaji wake kutokana na ratiba ya michezo kwa kusafiri kutoka Lindi, hali iliyosababisha kushuka kwa umakini na maamuzi mabaya uwanjani.

“Baadhi ya wachezaji walionekana kuishiwa nguvu na hilo lilisababisha kupungua kwa umakini wetu. Hata hivyo, tunajifunza kutokana na makosa hayo na tunaendelea kujipanga kwa michezo ijayo,” alisema Juma.

Kocha huyo alisisitiza kuwa licha ya matokeo hayo, Alliance Girls bado ina malengo makubwa katika ligi msimu huu, ikiwemo kuhakikisha inamaliza katika nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi.

“Timu yetu itaendelea kupambana hadi mwisho wa msimu. Lengo letu ni kumaliza katika nafasi nne za juu, na tunaamini bado tuna nafasi ya kufanya vizuri,” alisema.