UONGOZI wa Namungo uko katika hatua za mwisho kuipata saini ya beki wa kushoto wa Azam FC, Julius Machela kwa mkopo hadi mwisho wa msimu huu ikiwa ni siku chache tangu imsajili beki wa kati Ali Hassan Chamulungu kutoka kikosini humo.
Machela ni miongoni mwa nyota wanne wa akademi ya Azam waliojumuishwa katika kikosi cha wakubwa kilichoshiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026, akiungana na kipa, Shabani Juma, beki wa kushoto, Abdallah Mnumba na kiungo, Feisal Othman.
Akizungumzia suala hilo, Mratibu wa Namungo, Ally Suleiman, alisema tayari wamefanyia kazi ripoti ya benchi la ufundi kwa kuangalia maeneo ya kuboresha, ambapo muda wowote kuanzia sasa wataanza kutangaza mchezaji mmoja baada ya mwingine.
“Tumeanza na Ali Hassan Chamulungu, lakini hatutaishia hapo kwa sababu tunahitaji kuboresha kila eneo kutokana na ripoti ya benchi la ufundi, wachezaji wengine tuko nao hatua za mwishoni kukamilisha baadhi ya taratibu muhimu,” alisema Ally.
Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua Machela amejiunga na timu hiyo hadi mwisho wa msimu huu, akiungana na Ali Chamulungu, ambaye alisaini mkataba wa kuichezea Azam ya wakubwa Julai 24, 2025, utakaomweka ndani ya kikosi hicho hadi mwaka 2030.
Mbali na Machela na Chamulungu, Namungo imekamilisha usajili wa kipa Ahmed Feruz aliyekuwa Stand United ‘Chama la Wana’, kwa ajili ya kuongeza nguvu katika eneo hilo, huku nyota huyo akiwahi kuchezea pia timu za Simba na Kagera Sugar.
Nyota mwingine aliyejiunga na kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’ ni kiungo mshambuliaji wa Alliance FC ya jijini Mwanza inayoshiriki First League, Julius David Masuka.