Mbowe: Taifa bado lina maumivu makubwa

Arusha. Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema Taifa bado lina maumivu makubwa kutokana na hali ya kisiasa, akibainisha kuwa magereza yanaendelea kuwa na viongozi wanaostahili kuwa huru na kuungana na Watanzania wenzao katika kushuhudia na kuchangia matunda ya nchi yao.

Mbowe ameyasema hayo leo Jumamosi, Januari 24, 2026, wakati wa mazishi ya mwasisi wa Chadema, hayati Edwin Mtei, yaliyofanyika katika makaburi ya familia nyumbani kwake Tengeru, mkoani Arusha.

Akizungumza katika hotuba yake ya kwanza hadharani tangu aondoke rasmi kwenye uongozi wa Chadema na kustaafu siasa mwaka mmoja uliopita, Mbowe amesema kuna haja ya Taifa kujitafakari upya juu ya masuala ya uhuru, haki na maridhiano ya kweli kwa masilahi ya amani na maendeleo ya nchi.

Katika hotuba hiyo, Mbowe amemwomba Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, kuufikishia ujumbe wake kwa Rais (Samia Suluhu Hassan), akieleza kuwa Chadema iko tayari kushiriki katika ujenzi wa Taifa endapo itajiridhisha kuwa kuna nia ya dhati kutoka upande wa Serikali.

“Chadema wanataka kuijenga nchi hii. Tunataka kuona makundi yote yanapewa nafasi stahiki kwa mujibu wa Katiba ya nchi. Hakuna jambo la msingi kama uhuru wa watu katika nchi yao,” amesema Mbowe.

Amesisitiza kuwa maono ya hayati Mzee Mtei yalijikita katika kujenga Taifa lenye haki, demokrasia na usawa, akieleza kuwa kumuenzi kwa vitendo kunahitaji ujasiri wa kisiasa, maridhiano ya kweli na kuheshimu misingi ya kikatiba.

Kauli ya Mbowe imekuja katika mazingira ambayo mazishi ya Mzee Mtei yamekuwa jukwaa la viongozi mbalimbali kutoa tafakari pana kuhusu mustakabali wa demokrasia, umoja na maridhiano ya kitaifa, huku wakimtaja marehemu huyo kama alama ya msimamo, busara na mapambano ya amani kwa mageuzi ya kisiasa nchini.

Mbowe ambaye pia ni msemaji wa familia hiyo, akitoa neno la shukrani amesema ameamua kuyazungumza hayo leo ikiwa imepita muda wa mwaka mmoja na siku moja tangu astaafu rasmi siasa na kurudi kwenye biashara.

Mbowe ambaye muda wote wa hotuba yake alikuwa akishangiliwa, alianza kwa kueleza kuwa uwanja huo  umejaa makundi mwili yenye maumivu makubwa na kuwa yeye ambaye alimfahamu vizuri Mzee Mtei na amefanya naye kazi, alikuwa mtu mkweli asiyeyumba katika misimamo yake, lakini anayetekeleza ahadi zake.

“Waziri Mkuu utambue wewe na viongozi wa Serikali kwamba taifa letu bado lina maumivu makubwa sana nitakuwa mnafiki au mswahili nisipolisema hili. Maendeleo ambayo umetueleza kwamba Serikali itasimamia ni jambo jema tutashukuru lakini hakuna jambo la maana na muhimu kuliko uhuru wa watu katika nchi yao.

“Njia bora kuliko zote za kuleta maendeleo katika nchi, rejesheni kwanza uhuru wa watu, furaha ya watu, haki ya watu, na mkiri ukweli pale ambapo Serikali ilipokosea isione kusema ilikosea hapa turekebishe.”

Amesema anaamini hata  viongozi wa chama chake watakuwa tayari kuwasikiliza ili kuitafuta  kesho iliyo bora katika nchi.

“Chama. hiki kinaitwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, tukitambua pale pawapo na demokrasia ya kweli maendeleo yatapatikana. Waziri Mkuu maadamu umesema wewe ndiye umekabidhiwa jukumu hili la kuhakikisha kwamba taifa linatengemaa kasimameni na hili. Hiki chama ni chama ni chama kikuu kina mamilioni ya wanachama.

“Tengenezeni utaratibu wa makusudi wa kuyarekebisha na ninyi viongozi wote wa vyama vya upinzani tafuteni namna ya kufanya kazi pamoja ili katika utaratibu guo wa kuliunganisha Taifa hili lisiendelee kuwa na vipande vipande vya vyama vya siasa tunataka taifa moja lenye misingi ya maendeleo, lenye upendo ili hata watakaokuwa katika uongozi sehemu mbalimbali wafanye kazi yao kwfuraha na amani,” amesema na kuongeza;

“Nina imani kukutanishwa leo mbele ya msiba na jeneza la Mtei ni mpango wa Mungu na haya maneno tunayosema msitoke Serikali mkafikiri Chadema ni wakorofi, siyo wakorofi Chadema wameonewa wanapoonewa ni lazima wasimame kwa sababu ndicho tulichowafundisha katika chama hiki.Nimesema niyazungumze hayo mimi tangu nimestaafu sijasema mambo ya siasa. Na leo nina mwaka mmoja na siku moja tangu nistaafu rasmi siasa na kuridi kwenye biashara

“….Na wengi walihoji Mbowe amesimama upande gani ooh Mbowe,aaaaah…Ishu hapa siyo vyama vya siasa,ishu ni nchi yetu hawa viongizi siyo wakorofi wanalazimishwa kuwa wakorofi.Wanachadema,viongozi niwaite wadogo zangu tuitafute suluhu katika matatizo ya nchi yetu lakini hiyo nia njema ninayoomba muisimamie itakuwa kweli tu upande wa Serikali mtaonyesha dhamira ya kweli ,”

Awali, kabla ya Mbowe kuzungumza, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ambaye alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, ameeleza kuwa ameyapokea alliyosikia kwa niaba ya Serikali na bahati nzuri ‘political will’ (utashi wa kisiasa)  ipo na yeye ametumwa kusimamia na kuwahakikishia kuwa ameyapokea na  Serikali haitakuwa kikwazo cha kuhakikisha nchi inakuwa moja.

“Niwahakikishe Serikali haitakuwa kikwazo kuhakikisha nchi inakuwa moja na tunasonga mbele , tutavuka  na heshima ya Tanzania ya mara zote tutakuwa nayo,” amesema.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa Mzee Edwin Mtei aliyezikwa leo Jumamosi nyumbani kwake Tengeru wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha. Picha na Filbert Rweyemamu



Akimzungumzia Mtei amesema kuwa atakumbukwa kwa misimamo yake, ujasiri, maono, uvumilivu na kupenda nchi na amekuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza demokrasia ya vyama vingi.

Amesema Rais amemwelekeza kumuenzi Mzee Mtei kwa vitendo na ameagiza kusimamiwa ujenzi wa Barabara ya Arusha-Moshi (kipande cha Tengeru hadi Usa River), kwa kuhakikisha mchakato wa manunuzi kipande hicho unafanyika hata ili kuacha alama kumuenzi Mtei.

Amesema kipande cha kutoka Usa River hadi Kia (kilomita 28) ambacho usanifu wake umefika asilimia 80, kikamilishwe haraka  na kutangaza kandarasi ya ujenzi wa barabara hiyo ya njia nne ili kumuenzi Mtei kama mpenda maendeleo.

“Mzee Mtei alikuwa mpenda maendeleo, Rais amenielekeza mimi kama msimamizi niwaagize Mkuu wa Mkoa, Meya na Wakurugenzi wa halmashauri kubaini maeneo yanayofanyiwa biashara na wafanyabiashara wadogo, na kuyaboresha ili mazingira yawe rafiki kwa wafanyabiashara.

Akihubiri katika ibada ya maziko, Askofu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana, Saimon Makundi, amesema Mtei alikuwa mwadilifu hata yeye anashuhudia hayo.

“Alikuwa siyo mtu wa kupenda mambo ya ufisadi. Hata na wewe ukipewa nafasi ishi maisha kama ya mzee Mtei. Lazima kuzungumza pale mnapotofautiana ikiwa ni taifa au familia. Wako watu katika taifa letu mnawajua wanaweza kuleta upatanisho kama kuna shida.

“Hata kama tumekwama mahali na ninyi mnajua tusikae hapo tuende mbele, ndivyo inavyotakiwa katika taifa letu tukae tuzungumze katika haki na kweli na uwazo ili tuendelee mbele hata kama imetokea nini sisi ni binadamu,” amesema.

Amesema kuwa hata yeye katika uongozi wake ilifika mahali akakwama lakini ilibidi wazungumze kwa umakini na busara na jambo hilo likaisha.

“Mzee huyu maisha yake ya kiroho na kimwili aliishi kwa uadilifu, hivyo hata ukitofautiana na ndugu yako unaweza ukakaa nyumbani, msilale, msiache mkae mzungumze mtubu pale mlipokosea kwa sababu neno la Mungu linasema tukisema hatuna dhambi tunajidanganya.