Kiongozi wa CWT Morogoro afariki dunia kwa ajali

Morogoro. Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Morogoro kimepata pigo kufuatia kifo cha mwenyekiti wake, Mbaruku Ligubi (46), aliyefariki dunia baada ya kupata ajali ya barabarani iliyotokea usiku wa Januari 22, 2026.

Mwalimu Ligubi aligongwa na gari katika ajali iliyotokea saa 2 usiku katika barabara kuu ya Dar es Salaam – Morogoro, eneo la Shamba la Mkonge la Pangawe (Central Line) ambapo marehemu alikuwa akiendesha pikipiki akitokea Mkambarani kuelekea nyumbani kwake, Kingolwira.

Akizungumza na Mwananchi leo Januari 24, 2026, Katibu wa CWT Mkoa wa Morogoro, Alfonce Mbassa amesema kifo cha Ligubi ni pigo kwa familia, walimu na taasisi aliyokuwa akiitumikia kwa uadilifu mkubwa.

Mbassa amesema katika maisha yake ya utumishi, marehemu aliwahi kufundisha katika shule za msingi za Gezaulole, Kinole na Mkambarani na tangu mwaka 2015, alikuwa mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Morogoro.

Vilevile, amesema marehemu huyo alihudumu kama Ofisa Elimu Kata tangu mwaka 2020 hadi umauti ulipomfika, akianzia Mtombozi na baadaye Konde alikokuwa hadi dakika yake ya mwisho.

“Mwalimu Ligubi alikuwa kiongozi mchapakazi na mwenye kujali maslahi ya walimu. Ameacha pengo kubwa kwa familia, CWT na jamii nzima ya walimu,” amesema Mbassa, akiongeza kuwa marehemu ameacha mke na watoto watatu,” amesema Mbassa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkambarani, Ruben Chabaliko amesema muda mfupi baada ya tukio hilo, kulionekana gari aina ya Fuso likipita katika eneo hilo kwa mwendo kasi likiwa limezima taa, jambo lililozua mashaka kuwa huenda ndilo lililosababisha ajali hiyo.

Chabaliko amesema baadaye alithibitishiwa kuwa aliyefariki dunia ni Mwalimu Ligubi na polisi walifika eneo la tukio na kuupeleka mwili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro. 

Mke wa marehemu, Mwalimu Halima Karambo amesema alipata taarifa za kifo cha mume wake saa 3 usiku kutoka kwa majirani.

Mwalimu Halima amesema mawasiliano yao ya mwisho yalikuwa mchana wa siku hiyo ambapo walijadili ada ya watoto wao.

“Nilikuwa namtafuta katika simu, nafikiri baada ya tukio ule usiku, lakini haikupatikana, ndipo nikapewa taarifa za kifo chake,” amesema kwa masikitiko mke huyo wa marehemu.

Akitoa salamu za rambirambi, Rais wa CWT Taifa, Seleman Ikomba amewataka walimu kuendeleza mshikamano, upendo na umoja, akisisitiza kuwa chama hicho kinapaswa kubaki chombo cha kuwaunganisha walimu na si cha kuwagawanya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amethibitisha kutokea kwa tukio jeshi hilo na kwamba wanafanya uchunguzi ili kubaini chanzo kilichosababisha kutokea kwa ajali hiyo.