Kamati ya Bunge: Vijana wawezeshwe mitaji, zana za kazi

Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeitaka Serikali kuweka mifumo madhubuti ya kuwawezesha wahitimu wa vyuo vya ufundi stadi kupata mitaji na zana za kazi.

Kamati hiyo imebainisha kuwa vijana wengi hushindwa kutumia na kuendeleza ujuzi walioupata mara baada ya kuhitimu kutokana na ukosefu wa rasilimali hizo.

Imesisitiza kuwa uwezeshaji huo ni muhimu katika kuwafanya wahitimu kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za ajira na maendeleo ya kiuchumi, kwa kuwapa fursa ya kujiajiri na kuchangia kikamilifu katika uzalishaji na ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Akizungumza leo, Januari 24, 2026, wakati wa ziara ya wajumbe wa kamati hiyo wilayani Chemba, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Jumbe amesema upatikanaji wa mitaji na zana za kazi utawasaidia vijana kutumia ujuzi wao kikamilifu na kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za kijamii na kiuchumi kwa vitendo.

Jumbe amesema uwezeshaji huo utaongeza ajira binafsi, kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa kupitia sekta ya ufundi stadi.

 “Hatua za uwekezaji katika majengo na vifaa ni muhimu, lakini bila kuimarisha mitaala, kuwajengea uwezo wakufunzi na kuhakikisha mafunzo yanalingana na mahitaji ya sasa ya soko la ajira, matokeo chanya hayatafikiwa kikamilifu,” amesema.

Amesisitiza muhimu ubora wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi uendane na uwekezaji unaofanywa na Serikali, akisisitiza kuwa majengo, vifaa na mifumo ya Tehama lazima viambatane na mitaala ya kisasa, walimu wenye weledi na mafunzo yanayoendana na mahitaji halisi ya soko la ajira.

“Bila kuzingatia ubora, uwekezaji wa fedha  hautaleta matokeo yaliyokusudiwa, hivyo Veta inapaswa kuhakikisha kila rasilimali inayowekezwa inazalisha wahitimu wenye ujuzi unaoweza kutatua changamoto za kijamii na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa,” amesema.

Amesema vyuo vya Veta vimepiga hatua ikilinganishwa na miaka ya nyuma na hasa eneo la upanuzi wa miundombinu, wigo wa kozi, ubora wa mafunzo na usambazaji wa vyuo hadi ngazi ya wilaya.

Mjumbe wa Kamati hiyo Asha Baraka amesema Veta inapaswa kujiweka katika nafasi ya kuvutia vijana zaidi kujiunga na vyuo vya ufundi stadi, kwa kubuni mafunzo yanayojibu changamoto za kijamii kama vile  upatikanaji wa maji safi, nishati ya umeme, makazi bora na huduma za msingi.

Asha amesema kuna haja kwa Veta kuwekeza katika mafunzo ya ufundi viatu vinavyokidhi mahitaji ya Watanzania wa makundi yote, kwani mafunzo hayo yakiandaliwa kwa kuzingatia mazingira ya ndani, kipato cha wananchi na ubora wa bidhaa, vitawasaidia vijana kuzalisha bidhaa bora.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, ufundi wa viatu unaweza kuunganishwa na ubunifu wa kisasa na matumizi ya malighafi za ndani, hivyo kuwa chanzo cha ajira na mapato kwa vijana katika maeneo ya vijijini.

Naye Bakar Shingo, ameshauri kuboreshwa kwa miundombinu ya maji katika chuo hicho na ujenzi wa uzio ili kuimarisha usalama wa wanafunzi na mali za chuo.

Pia, ametaka zianzishwe kozi zinazozingatia mazingira ya Wilaya ya Chemba na katika vyuo vingine kuwe na utamaduni wa namna hiyo kwani wanaosoma wanatoka katika mazingira hayo.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta),  Anthon Kasore, amesema katika kuimarisha upatikanaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa usawa wameboresha na kuwa na ubunifu na kuzalisha rasilimali watu wenye umahiri na weledi.

Amesema katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2026, jumla ya wanafunzi 430,416 wamedahiliwa katika vyuo vya VETA nchini, wakiwemo 1,830 wenye mahitaji maalum na 6,515 wanaotoka katika mazingira magumu.

Kasore ameongeza kuwa Veta inaendelea kushirikiana na PPRA ili kuhakikisha vikundi vya wahitimu vinapata usajili rasmi, fursa za ujasiriamali pamoja na vitendea kazi, hatua itakayowawezesha kuingia sokoni na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.