Dar es Salaam. Kama ni kumng’ang’ania mtu basi aliyekuwa mgombea ubunge Chamazi kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Kondo Bungo anaendelea kufanya hivyo hivyo kwa Mbunge wa Jimbo hilo, Abdallah Chaurembo.
Safari hii si kwenye korido za kisiasa kama ilivyokuwa wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025 ambapo Chaurembo alitangazwa mshindi kupitia CCM, safari hii ni mtifuano wa kisheria kortini ambapo Bungo amefanikiwa kuvuka kiunzi cha kwanza.
Hii ni baada ya Jaji Arnold Kerekiano wa Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, kulitupa pingamizi la awali lililowekwa na walalamikiwa watatu katika shauri la uchaguzi namba 30591 la mwaka 2025.
Bungo amefungua shauri hilo dhidi ya Chaurembo kama mlalamikiwa wa kwanza, Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Chamazi Jijini Dar es Salaam kama mlalamikiwa wa Pili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kama mlalamikiwa wa tatu.
Mgombea huyo kwa tiketi ya ACT Wazalendo anaiomba mahakama pamoja na mambo mengine, itoe amri ya kubatilisha uchaguzi wa jimbo hilo kwa nafasi ya ubunge kwa hoja kuwa uchaguzi huo ulikuwa batili.
Hata hivyo, mlalamikiwa wa kwanza kupitia kwa wakili wake, Bernard Maguha, pamoja na hatua nyingine alizochukua, aliweka pingamizi la awali.
Katika pingamizi hilo, alieleza kuwa shauri hilo halina uhalali kisheria kwa kuwa limefunguliwa nje ya siku 30 baada ya kutangazwa kwa matokeo kinyume na kifungu 144(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na Madiwani ya 2024.
Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi, Bungo aliwakilishwa na mawakili Juma Nassoro na Daimu Khalfan wakati Chaurembo aliwakilishwa na Maguha, Msimamizi wa uchaguzi na AG waliwakilishwa na wakili wa Serikali, Narindwa Sekimanga.
Kulingana na uchambuzi wa Jaji Kirekiano katika uamuzi wake mdogo, amesema mawakili wa pande zote mbili walikuwa na msimamo wa pamoja kuwa matokeo ya uchaguzi wa Jimbo la Chamazi yanayobishaniwa yalitangazwa Oktoba 30, 2025.
Pili, wanakubaliana ni takwa la kisheria shauri la uchaguzi linapaswa kuwasilishwa ndani ya siku 30 tangu kutangazwa kwa matokeo na kwamba shauri lililiwasilishwa mahakamani Desemba 1, 2025 na taratibu za usajili kukamilika siku iliyofuata.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Jaji, mawakili hao walikuwa wanatofautiana mtizamo katika kuhesabu siku 30 tangu matokeo ya uchaguzi, yaani Oktoba 30, 2025 na kama hiyo tarehe ijumuishwe au iondolewe katika kukokotoa siku 30.
Wakili Maguha anayemwakilisha Chaurembo alijenga hoja kuwa sheria aliyoinukuu awali inataka mtu mwenye nia ya kupinga matokeo, anaweza kufanya hivyo ndani ya siku 30 kuanzia tarehe matokeo ya ubunge yalipotangazwa.
Hoja yake ilikuwa ni kwamba maneno “kuanzia tarehe ya kutangazwa matokeo”, yalikusudiwa kujumuisha siku ya kutangazwa matokeo na kwa sababu hiyo siku 30 zinaishia Novemba 28, 2025 ambayo ilikuwa siku ya Ijumaa na ni siku ya kazi.
Wakili huyo alikuwa na hoja kuwa kwa kuwa shauri hilo liliwasilishwa mahakamani Desemba 1, 2025, hii ina maana kwamba liliwasilishwa mahakamani siku tatu baadaye, hivyo liliwasilishwa nje ya muda kinyume na kifungu kile cha 144(1).
Hata hivyo, Wakili Nassoro aliyemwakilisha Bungo alipinga hoja hiyo akisema neno “kuanzia” lililotajwa, halijatafsiriwa na sheria husika, hivyo mahakama itumie tafsiri kutoka Sheria ya Tafsiri ya Sheria, kifungu cha 61(1)(b) kinachoeleza:-
“Pale ambapo kipindi cha muda kinaonyeshwa kuhesabiwa kutoka, au baada ya, siku iliyotajwa siku hiyo haitajumuishwa katika kipindi hicho”.
Kwa sababu hiyo, wakili huyo alisema ukiondoa siku ya tukio, yaani Oktoba 30, 2025, siku 30 zinaangukia Novemba 29, 2025 ambayo ilikuwa siku ya Jumamosi na sheria inasema ikiangukia siku si ya kazi, jambo litafanywa siku inayofuata ya kazi.
Hivyo, wakili huyo alijenga hoja kuwa kwa kuwa siku ya kazi iliyofuata ni Desemba 1, 2025 na shauri hilo liliwasilishwa siku hiyo, basi shauri liliwasilishwa ndani ya muda na ielewe nyaraka itahesabika imesajiliwa siku itakapowasilishwa.
Katika uamuzi wake, Jaji alisema hakuna ubishi juu ya msimamo wa sheria kwamba shauri la uchaguzi ni lazima liwasilishwe ndani ya siku 30 tokea matokeo ya uchaguzi yalipotangwa na katika Jimbo hilo yalitangazwa Oktoba 30, 2025.
“Kwa sababu hiyo, kuhesabu siku 30 kumeibua hoja ambayo ndio msingi wa uamuzi huu, ikiwa tarehe Oktoba 30, 2025 ijumuishwe au iondolewe na hatimaye siku 30 zihesabiwe kuanzia tarehe Oktoba 31, 2025,” alisema Jaji Kirekiano.
“Ili kuweka msingi mzuri katika kujibu mitizamo tofauti ya mawakili, ni vema kurejea katika kifungu husika kinachoweka ukomo wa muda yaani kifungu cha 144 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya 2024.
Alisema mawakili wanatofautiana tafsiri ya maneno “kuanzia tarehe ya kutangazwa kwa matokeo”, na kwa kuwa ni jukumu la Mahakama kutafsiri sheria hivyo ataegemea uamuzi wa shauri la Monica Mgaya dhidi ya Ali Damji.
Shauri hilo aliliweka msimamo wa kisheria kuwa “Kukokotoa kikomo cha muda ni zoezi la kisheria kuliko nambari tu. Tafsiri pana inapaswa kufanywa katika tafsiri, kwa kuzingatia sheria zote zinazohusika.”
“Kwa ufupi niseme ni mtizamo wangu maneno “kuanzia” ambayo ndiyo tafsiri ya moja kwa moja ya neno “from” ni maneno kisawe, ambayo yanaakisi malengo ya kifungu cha 61 cha sheria ya tafsiri ya kuondoa siku ya kwanza,” alisema Jaji.
“Kwa sababu hiyo, nakubaliana na hoja za Wakili Nassoro (wa mdai) kwamba kwa msingi wa sheria ya tafsiri, siku 30 zitapaswa kuhesabiwa kuanzia tarehe Oktoba 31, 2025. Baada ya kufanya hivyo, siku 30 zitaishia tarehe Novemba 29, 2025”
Jaji akaongeza: “Ikumbukwe kuwa siku hiyo ilikuwa ni Jumamosi na tarehe 30 ilikuwa ni Jumapili. Kwa kuwa nyaraka za shauri hili ziliwasilishwa tarehe Desemba 1, 2025 na zikakamilika na kulipiwa ada Desemba 2, 2025, mahakama imeangalia suala hili lisilobishaniwa, lakini ni vema ikaweka kumbukumbu sawa.”
“Mosi, kwa kuwa tarehe 29 na 30 Oktoba 2025 hazikuwa siku za kazi, siku hizi zinapaswa kutozingatiwa katika hesabu ya ukomo. Hii ni kwa sababu siku ya mwisho iliishia siku isiyo ya kazi,” alisisitiza Jaji Kirekiano katika uamuzi wake.
“Msingi wake ni kifungu cha 61(2) cha sheria ya Tafsiri ya Sheria inayoelekeza kwamba endapo siku ya mwisho imeangukia siku ya sikuu au siku ya mwisho wa wiki basi siku hiyo ya mwisho iondolewe,”alisema Jaji na kuongeza;-
“Pili ikumbukwe kwamba shauri hili liliwasilishwa Desemba mosi, 2025 na kulipiwa ada Desemba 2, 2025. Kwa mujibu wa Kanuni ya 8 ya Kanuni za mashauri ya uchaguzi inaelekeza hati ya shauri itawasilishwa ndani ya siku 30”.
“Sasa uwasilishaji shauri unahusisha ulipaji ada, nimerejea sheria ya ufunguaji mashauri kwa njia ya mtandao na ulipaji ada. Kwa kuwa shauri liliwasilishwa tarehe Desemba mosi, 2025, taratibu za ulipaji zingeweza kukamilika ndani ya siku saba”
“Kwa msingi huo na kwa ujumla wa yale niliyoyaeleza hapo juu, nakubaliana na hoja za wakili wa mlalamikaji kwamba pingamizi lililowasilishwa halina mashiko, shauri hili liliwasilishwa ndani ya muda hivyo pingamizi linatupiliwa mbali”.
Jaji akasema amri juu ya gharama zitaamuliwa mbeleni wakati wa kukamilika kwa shauri hilo na usikilizwaji wa awali umepangwa kufanyika Januari 30, 2026.