CCM Pwani: Malezi bora ni nguzo ya amani

Kibaha. Wazazi mkoani Pwani wametakiwa kuimarisha malezi kwa vijana ili kuwajengea misingi ya amani, nidhamu na uzalendo, huku wakihimizwa kuepuka vitendo vya vurugu vinavyoweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi.

Wito huo umetolewa leo Jumamosi, Januari 24, 2026, na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hamoud Abuu Jumaa, wakati wa kikao cha Baraza la Umoja wa Wazazi Mkoa wa Pwani kilichofanyika mjini Kibaha.

Akizungumza katika kikao hicho, Abuu Jumaa amesema amani ni rasilimali muhimu kwa Taifa na msingi wa maendeleo endelevu, akisisitiza kuwa bila amani hakuna jitihada za maendeleo zinazoweza kuzaa matunda.

“Amani ni mtaji mkubwa wa Taifa. Ni bora hata kuliko afya, kwa sababu bila amani huwezi kujenga wala kuendeleza chochote. Wazazi mna jukumu kubwa la kuwalea vijana wenu wawe walinzi wa amani hii,” amesema.

Katika hatua nyingine, amewahimiza vijana kuwekeza zaidi katika elimu na maarifa ili waweze kushindana katika soko la ajira na kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazojitokeza ndani na nje ya nchi.

Awali, Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi Mkoa wa Pwani, Josiah Kituka, amewataka wanachama wa umoja huo kufanya kazi kwa upendo, mshikamano na uvumilivu, akisisitiza umuhimu wa kuepuka makundi na visasi, hususan kwa wale waliogombea nafasi za uongozi na kutopata ushindi.

“Ni muhimu tukafanya kazi kwa umoja. Tusiwe na chuki wala visasi, maana kila jambo hutokea kwa wakati na kwa mapenzi ya Mungu,” amesema Kituka.

Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Pwani, Kite Adamu Mfilinge amesema chama kitaendelea kujengwa juu ya misingi ya umoja na ushirikiano, akibainisha kuwa mshikamano miongoni mwa wanachama ni silaha muhimu katika kuimarisha chama na kuwatumikia wananchi kwa ufanisi.

Kwa upande wake, mkazi wa Kibaha, Amina Shabani amesema Serikali inapaswa kuendelea kuweka mipango mahsusi ya kuwawezesha vijana katika nyanja mbalimbali, ikiwemo elimu, ajira na uongozi, ili kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

Kauli hizo zimetolewa katika kipindi ambacho wadau mbalimbali wameendelea kusisitiza umuhimu wa malezi bora, elimu na amani kama nguzo kuu za ustawi wa jamii na maendeleo ya nchi.