Madiwani Wanging’ombe wawataka wanawake kuacha kutumia uzazi wa mpango

Njombe. Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe wamependekeza wanawake kuacha kutumia uzazi wa mpango wakidai hatua hiyo imechangia kupungua kwa idadi ya watoto, hali iliyosababisha kushuka kwa uandikishaji wa wanafunzi katika shule za awali na msingi wilayani humo.

Pendekezo hilo limetolewa mwishoni mwa wiki wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani cha kujadili na kupitisha rasimu ya bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe, ambapo suala la upungufu wa watoto walioandikishwa shule lilijadiliwa kwa kina.

Madiwani wamesema katika tathmini yao, elimu ya uzazi wa mpango imewafikia wananchi wengi na kusababisha kupungua kwa kasi ya uzazi, jambo linaloathiri idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule pamoja na mustakabali wa nguvu kazi ya baadaye wilayani humo.

Mmoja wa madiwani hao, Annaupendo Gombela wa Kata ya Mdandu, amesema Baraza la Madiwani limeona umuhimu wa kuhamasisha wanawake kuacha kutumia uzazi wa mpango ili kuongeza idadi ya watoto na nguvu kazi ya baadaye.

“Kuwa na idadi kubwa ya watu kunasaidia siyo tu kupata watoto watakaosoma, bali pia kuimarisha nguvu kazi na kuongeza mapato ya Serikali kupitia mchango wa wananchi katika shughuli za maendeleo,” amesema Gombela.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe, Agnetha Mpangile, amesema kuna haja ya madiwani na viongozi wa jamii kukaa na wananchi ili kuhamasisha suala la uzazi, huku akibainisha kuwa changamoto za kifamilia pia zinachangia baadhi ya wanawake kuamua kupunguza idadi ya watoto.

“Ipo haja ya kuchukua hatua ili watu wazaliane, lakini ukiwauliza akina mama wanasema sababu kubwa ni baadhi ya wanaume kutotekeleza wajibu wao wa kuhudumia familia,” amesema Mpangile.

Hata hivyo, maoni ya wananchi kuhusu uzazi wa mpango yameonekana kugawanyika, ambapo baadhi wakiutetea wakisema unasaidia kuboresha malezi na ustawi wa watoto.

Mkazi wa Njombe, Shabani Ramadhani, amesema uzazi wa mpango unasaidia kupanga familia na kuhakikisha kila mtoto anapata malezi bora kutokana na kuwepo kwa nafasi ya kutosha kati ya mtoto mmoja na mwingine.

“Uzazi wa mpango unasaidia kila mtoto kupata uangalizi mzuri kwa sababu mzazi ana uwezo wa kuwahudumia kulingana na kipato chake,” amesema Ramadhani.

Naye Winifrida Msalilwa amesema uzazi wa mpango unapaswa kuendelea kuwepo kwa kuwa unawasaidia wazazi kuwapatia watoto elimu na lishe bora, akionya kuwa kuzaa watoto wengi bila uwezo kunaweza kusababisha changamoto za kiafya ikiwemo utapiamlo na udumavu.

“Ni bora uzazi wa mpango uendelee ili wazazi waweze kuwalea watoto wanaowazaa kwa ubora, badala ya kuzaa wengi wasioweza kuwamudu,” amesema Msalilwa.

Mjadala huo unaibua hoja pana kuhusu uwiano kati ya ongezeko la watu, uwezo wa familia, elimu, afya na maendeleo endelevu katika jamii.