Wizara ya Viwanda yataja mikakati 12, vijana watajwa

Dodoma. Kuelekea siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan madarakani tangu alipoapishwa kwa muhula wake wa pili, Wizara ya Viwanda na Biashara imetaja mambo 12 ambayo yamepewa mkazo mkubwa ikiangazia kundi la vijana.

Katika kutekeleza mipango hiyo, mikopo 193 yenye thamani ya zaidi ya Sh820 milioni imetolewa na kuzalisha ajira 546, mingi ikiwagusa vijana. 

Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga ametoa takwimu hizo leo Jumamosi Januari 24, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa babari kuhusu mkakati wa mafanikio ya siku 100 za Rais Samia.

Tume ya Taifa ya uchaguzi ilimtangaza Samia Suluhu Hassan (CCM) kuwa mshindi wa kiti cha Rais kwenye matokeo ya Novemba Mosi, 2025 na Novemba 3, 2025 aliapishwa katika viwanja vya Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Miongoni mwa mambo yaliyotajwa ni uwezeshaji wa wajasiriamali wadogo na wa kati, uendelezaji wa mitaa ya viwanda na programu maalumu za vijana.

Mengine ni uongezaji thamani kupitia viwanda, uvutiaji wa uwekezaji wa viwanda na urasimishaji wa biashara na miliki ubunifu.

“Lakini mengine ni mafunzo na uatamizi wa biashara kwa vijana, ubora wa bidhaa kwa wajasiriamali taarifa masoko na biashara za kimataifa na uwezeshaji wa mauzo ya korosho,” amesema Kapinga.

Mikakati mingine ni muungano wa kampuni na ukuaji wa mitaji, utafiti wa madini adimu na ya kimkakati (Tirdo) pamoja na uchumi wa kijani na nishati safi. 

Waziri amesema ndani ya siku hizo, mitaa ya viwanda na kongani zimezalisha maelfu ya ajira na kuandaa programu ya biashara 100,000 za vijana ambapo vijana 1,200 wamepata mafunzo ya ujasiriamali na kuingizwa kwenye programu za uatamizi wa biashara. 

Kwenye taarifa hiyo, amesema miradi ya mpira Kalunga, mkaa mbadala na tafiti za madini adimu imeimarisha msingi wa uchumi wa kijani na uchumi wa kimkakati.

Akizungumzia agizo la Waziri Mkuu kuhusu biashara zinazoweza kuendeshwa na wazawa lakini zina wageni, amesema amesema wanaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ikiwemo katika masoko makubwa ya Kariakoo.

“Lakini Brela wamepewa maelekezo wakati wa usajili wa biashara kuwa makini ili wasitoe usajili kwa wasiokuwa wazawa kwenye biashara ambazo zinaweza kumilikiwa na wazawa,” ameeleza Kapinga.

Waziri ametaja sekta binafsi kuwa imekuwa injini ya uzalishaji wa viwanda na kutoa ajira, hivyo Serikali inaendelea kutoa unafuu ili wakuze mitaji.