KOCHA wa Yanga, Pedro Goncalves amesema kikosi hicho kinaendelea kukua na hakitakata tamaa licha ya kupoteza ugenini dhidi ya Al Ahly kwa mabao 2-0 katika mechi ya tatu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Goncalves amesema huo ulikuwa mchezo wake wa 12 tangu aanze kuinoa Yanga, na ndiyo mara ya kwanza timu hiyo kupoteza chini ya uongozi wake huku akieleza kuwa kipigo hicho ni sehemu ya ukuaji wa timu.
Hata hivyo, Mreno huyo amesema hawajamalizana na vigogo hao wa Afrika na ili wafikie ndoto zao kubwa, lazima wawashinde.
“Timu inaendelea kukua. Ulikuwa mchezo wangu wa 12 nikiwa na Yanga na huu ndio ulikuwa mchezo wa kwanza kupoteza. Hii sio aibu kwetu. Tulitaka zaidi na hiyo ndiyo nguvu yetu kubwa, hatukati tamaa,” amesema Goncalves.
Kocha huyo raia wa Ureno, amekiri kuwa kipigo hicho kilikuwa kama pigo la ghafla kwa timu yake, lakini akasema hilo haliwezi kuwavunja moyo kwani bado wana ndoto kubwa za kufanya vizuri kwenye mashindano ya Afrika.
“Ndiyo, tulipigwa kama ngumi, lakini kesho ni siku nyingine. Tunapaswa kujiuliza kama tumekufa au bado tunaishi kwa ajili ya malengo makubwa tuliyojiwekea. Lengo letu kubwa ni kuvuka hatua ya makundi,” ameongeza.
Goncalves alibainisha kuwa, tangu mwanzo Yanga haikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kufuzu, kutokana na kuingia kwenye kundi gumu lenye mabingwa wa Afrika, lakini hilo haliwakatishi tamaa.
“Hatukuwa tukipewa nafasi tulipoingia kwenye kundi lenye Al Ahly, FAR Rabat na Kabylie, timu zote ambazo ni mabingwa wa Afrika. Sisi ni timu pekee kwenye kundi ambayo haijawahi kuwa bingwa wa Afrika, lakini hilo halimaanishi hatuwezi kupambana. Tunaendelea kukua na tunaweka malengo makubwa,” amesema.
Kocha huyo ameeleza kuwa, ili Yanga ifikie ndoto zake kubwa, haina budi kuwashinda vigogo wa soka la Afrika, akiahidi kuwa timu hiyo itaendelea kupigana hadi mwisho wa mashindano.
Licha ya Yanga kupoteza kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Mahmoud Hassan ‘Trezeguet’, takwimu za mchezo huo uliochezwa Januari 23, 2026 kwenye Uwanja wa Borg El Arab nchini Misri zinaonesha wazi haikuwa mechi rahisi kwa Al Ahly, kwani Yanga iliingia kwa ushindani mkubwa dhidi ya mabingwa hao wa Afrika mara 12.
Al Ahly ilimiliki mpira kwa asilimia 57 dhidi ya 43 za Yanga, huku Yanga ikijaribu kujilinda kwa umakini mkubwa hasa dakika 45 za kipindi cha kwanza na kushambulia kwa kushtukiza.
Katika upigaji wa mashuti, Al Ahly ilipiga 10 dhidi ya 9 ya Yanga, lakini Yanga ililenga lango mara nne ikilinganishwa na mashuti matatu yaliyolenga lango kwa Al Ahly, jambo linaloonesha ujasiri wa safu ya ushambuliaji ya Wananchi.
Tofauti kubwa ilijitokeza kwenye ubora wa nafasi, ambapo Al Ahly ilikuwa na uwezekano wa kufunga bao 1.02 dhidi ya 0.33 ya Yanga, hali inayoakisi ufanisi wa Al Ahly katika kutumia nafasi chache ilizozipata.
Yanga ambayo ipo nafasi ya pili katika msimamo wa kundi B ikiwa na pointi nne, inarejea nyumbani Tanzania kwa ajili ya mechi ya nne katika hatua hiyo ambapo itapigwa wikiendi ijayo huko Zanzibar dhidi ya Al Ahly kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.
Kocha huyo aliyeanza kazi rasmi kuiongoza Yanga Oktoba 28, 2025, ameshinda mechi kumi za mashindano tofauti, sare moja na kupoteza moja, huku akibeba Kombe la Mapinduzi 2026.
Katika mechi hizo 12 Ligi Kuu Bara (5), Kombe la Mapinduzi (4) na Ligi ya Mabingwa Afrika (3).