Azam, Singida BS kanyaga twende CAFCC

WAWAKILISHI wa nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Azam na Singida Black Stars wanashuka viwanjani leo kupambana kujiweka katika nafasi nzuri kuwania kufuzu robo fainali.

Azam itakuwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Nyayo huko Kenya kucheza dhidi ya Nairobi United saa 10:00 jioni, huku timu zote mbili msimu huu zikiweka rekodi ya kufuzu hatua ya makundi michuano ya CAF kwa mara ya kwanza.

Azam iliyochapwa mechi zote mbili ikiwa nafasi ya tatu kundi B, inahitaji ushindi wa aina yoyote ili kuweka hai matumaini yatakayoamsha morali kikosini kabla ya timu hizo kurudiana wiki ijayo Zanzibar.

Timu hiyo iliyofuzu hatua ya makundi ya michuano ya CAF kwa mara ya kwanza katika historia yake, ilichapwa mabao 2-0 dhidi ya AS Maniema Union ya DR Congo, kisha mechi ya pili ikapoteza kwa bao 1-0 mbele ya Wydad Casablanca ya Morocco.

Azam iliandika rekodi katika michuano ya CAF baada ya kufuzu makundi ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza tangu ianzishwe Julai 23, 2004 ikifahamika Mzizima FC.

Timu hiyo iliyopanda Ligi Kuu Julai 27, 2008 imeweka rekodi hiyo chini ya Kocha Mkongomani Florent Ibenge aliyejiunga nayo Julai 5, 2025 akitokea Al Hilal Omdurman ya Sudan.

Kwa upande wa Nairobi United iliandika pia historia ya kufuzu kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiing’oa kwa penalti 7-6, bingwa wa zamani wa CAF, Etoile du Sahel kutoka Tunisia, baada ya sare ya mabao 2-2.

Timu hiyo iliyoanzishwa mwaka 2015, ikifahamika kwa jina la Balaji EPZ kabla ya kubadilishwa mwaka 2022 na kuitwa Nairobi United, ipo mkiani mwa kundi hilo, baada ya kuchapwa pia mechi zote mbili ilizocheza msimu huu.

Nairobi United ilianza hatua ya makundi kwa kuchapwa mabao 3-0 dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco, kisha kufungwa bao 1-0 na AS Maniema Union ya DR Congo, huku timu zote zikikutana zikiwa hazijafunga bao lolote.

Ibenge alinukuliwa akisema baada ya mechi ya mwisho ya Ligi Kuu dhidi ya Fountain Gate iliyomalizika kwa suluhu ilikuwa ni njia mojawapo ya maandalizi muhimu ndio maana alifanya mabadiliko pia kwa baadhi ya wachezaji.

Mechi nyingine itakayopigwa leo saa 1:00 usiku, Singida inayoburuza mkia kundi C na pointi moja itakuwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja kuikaribisha AS Otoho ya DR Congo iliyo nafasi ya pili baada ya kukusanya pointi zake tatu.

Kocha wa Singida Black Stars, Mkenya David Ouma alisema changamoto kubwa anayopambana nayo katika kikosi hicho ni eneo la ushambuliaji, kwani licha ya kutengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini utulivu sio mzuri wa kuzibadilisha kuwa mabao. “Mechi yetu ya mwisho ya Ligi Kuu tuliyopoteza bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania tulitengeneza zaidi ya nafasi tano za wazi kipindi cha kwanza ingawa hatukuzitumia vizuri, mashindano ni tofauti hivyo, tunahitaji kuongeza umakini,” alisema Ouma.