Okello awaamsha mashabiki Yanga | Mwanaspoti

ACHANA na matokeo ya kupoteza kwa kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Al Ahly. Mashabiki na wanachama wa Yanga mkoani Mbeya, wamesema hawaidai chochote timu yao, huku wakieleza kuridhishwa na kiwango cha nyota mpya, Allan Okello.

Wamesema baada ya matokeo hayo, kwa sasa wanajiandaa kuisapoti timu hiyo itakaposhuka tena uwanjani kuwakaribisha wapinzani hao katika mchezo wa nne wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Jana Ijumaa, Yanga ilipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Al Ahly huko nchini Misri, na sasa itawakaribisha Waarabu hao Januari 31, 2026 visiwani Zanzibar ikiwa ni mechi ya kundi B.

Mratibu wa timu hiyo mkoani Mbeya, Said Komba ‘Kastera’ amesema licha ya matumaini waliyokuwa nayo, lakini wanakubaliana na matokeo kwani vijana walijituma na kutimiza wajibu wao na kilichotokea ni sehemu ya mchezo.

Amesema kwa sasa wameshaandaa mabasi mawili kwa ajili ya safari kuelekea Zanzibar kuisapoti timu yao kuhakikisha inashinda ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu robo fainali ya michuano hiyo.

“Okello ametuonesha kitu cha tofauti, usajili wa staa huyo utatulipa zaidi, nadhani aliyeangalia mpira atakubaliana na mimi kiwango cha nyota huyo, sisi mashabiki hatuwadai Yanga, walipambana.

“Al Ahly wanafungika, ni vile hatukupata bahati ila nafasi tulizopata, kilichobaki Yanga inahitaji mchezaji wa 12 na sisi Mbeya kwa kutambua umuhimu wa mechi hiyo tutaondoka mashabiki 60 kwenda kuongeza nguvu,” alisema Kastera.

Naye shabiki wa timu hiyo tawi la Iduda, Moses Mwasanga alisema kiwango kilichoonyeshwa na Yanga ni dalili za timu hiyo kuhitaji nafasi ya kufuzu hatua inayofuata iwapo watakaza Januari 31.

Katika usajili wa dirisha hili dogo mbali na Okello anayecheza winga, Yanga imewasajili Hussein Masalanga (kipa), Mohamed Damaro (kiungo mkabaji), Emmanuel Mwanengo (mshambuliaji), Laurindo Dilson Maria Aurélio ‘Depu’ (mshambuliaji), huku beki wa kulia Kouassi Yao akirudishwa.