Katika jamii nyingi, bado kuna imani iliyojikita kuwa ili uhusiano au ndoa idumu, lazima mmoja awe na mamlaka ya kuogopwa.
Kauli kama “mke anapaswa kumuogopa mumewe” au “lazima uwe mkali ili aheshimu” zimekuwa zikienezwa kwa vizazi.
Lakini sayansi ya uhusiano na utafiti vinaonyesha wazi kuwa hofu si msingi wa uhusiano wenye afya. Kinachodumisha ndoa au uhusiano si kuogopana, bali kuheshimiana.
Hofu huzaa ukimya, unafiki na kujisitiri. Heshima, kinyume chake, huzaa usalama wa kihisia, uaminifu na ukweli, kama makala haya yanavyoangazia kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya kimtandao.
Dk John Gottman, mtafiti mashuhuri wa ndoa, anaeleza kuwa uhusiano unaodumu kwa muda mrefu hujengwa juu ya misingi ya heshima na kuthaminiana, si vitisho wala mamlaka ya woga.
Anasema: “Bila heshima na kuthaminiana, uhusiano hauwezi kuishi kwa muda mrefu.” Kauli hii inaweka wazi kuwa heshima si pambo la ndoa, bali ni mhimili wake.
Uhusiano unapojengwa juu ya hofu, mmoja hulazimika kunyenyekea, kuficha hisia au kujibadilisha ili kuepuka adhabu ya kihisia au kimwili.
Kwa nje, uhusiano unaweza kuonekana mtulivu, lakini ndani kuna hofu, majeraha na umbali wa kihisia.
Heshima, kwa upande mwingine, hujenga mazingira ambayo kila mmoja ana uhuru wa kuwa yeye mwenyewe bila kuadhibiwa kwa kusema ukweli.
Dk Sue Johnson, mtaalamu wa tiba za kihisia anaeleza kuwa msingi wa uhusiano wa karibu ni usalama wa kihisia.
Usalama huo hauwezi kuwepo pale mmoja anapomwogopa mwenzake.Anasema hofu humfanya mtu ajilinde badala ya kufunguka, na uhusiano unapoteza ukaribu wake wa kweli.
Katika kitabu chake Hold Me Tight, Dk Johnson anaandika: “Uhusiano wenye afya ni ule ambao wenza wanahisi wako salama kwa kila mmoja.”
Kauli hii inaonyesha kuwa usalama wa kihisia ni sharti la msingi la upendo. Pale ambapo kuna hofu ya kukemewa, kudhalilishwa au kuachwa, usalama huo hutoweka, na uhusiano hubaki juu juu.
Hofu mara nyingi hujificha katika sura ya nidhamu, uongozi, au mila. Lakini athari zake ni zile zile: mmoja hunyamaza, mwingine hutawala.
Dk Johnson anaeleza kuwa katika mazingira ya hofu, migogoro haisuluhishwi bali huzikwa. Hisia hazizungumzwi, mahitaji hayasemwi, na hatimaye uhusiano hujaa hasira iliyofichwa.
Heshima, kinyume chake, hutoa nafasi ya migogoro kujadiliwa bila kuharibu uhusiano.
Bell Hooks, mwandishi na mwanafalsafa wa masuala ya upendo, anaweka wazi tofauti kati ya upendo wa kweli na udhibiti unaojificha kama upendo.
Katika kitabu chake All About Love, anaandika: “Upendo na hofu haviwezi kuishi pamoja.”
Tafsiri hii ina maana nzito sana: pale ambapo kuna hofu, upendo wa kweli hauwezi kustawi. Kinachobaki ni utegemezi, udhibiti au mazoea, si uhusiano wa heshima.
Hooks anaeleza kuwa jamii imechanganya dhana ya upendo na umiliki. Mmoja anapomdhibiti mwenzake kwa hofu, huweza kudhani anamlinda au kumpenda, ilhali kwa kweli anavunja utu wake.
Upendo wa kweli, kwa mujibu wa Hooks, unahitaji heshima, haki na usawa wa kihisia. Bila heshima, uhusiano hubadilika na kuwa mfumo wa nguvu badala ya muunganiko wa mioyo.
Emerson Eggerichs, mwandishi wa Kitabu: Love & Respect, anaeleza kuwa heshima ni hitaji la msingi katika uhusiano, hasa pale ambapo wenza wanatofautiana au wanapokosa kuelewana.
Anaeleza kuwa watu wengi huchanganya heshima na hofu, wakidhani kuwa mwenza anayenyamaza au anayenyenyekea ana heshima.
Lakini Eggerichs anaonya dhidi ya dhana hiyo akiandika: “Heshima ya kweli haihitaji hofu; hukua katika mazingira ya hiari na kuthaminiana.”
Kauli hii hii inaonyesha kuwa heshima haiwezi kulazimishwa. Pale inapolazimishwa, hubadilika na kuwa utii wa hofu, si heshima ya dhati. Heshima ya kweli hutokana na kutambua utu na thamani ya mwenzako.
Kwa mujibu wa Dk Gottman, ishara mojawapo ya uhusiano unaovunjika ni kudharau, kejeli na lugha ya kumdhalilisha mwenza.
Anaandika: “Dharau ni adui mkubwa wa uhusiano.” Hii inaonyesha kuwa pale ambapo heshima inapotea, hata kama hakuna hofu ya wazi, uhusiano huanza kufa taratibu. Dharau humfanya mwenza ajihisi mdogo, hafai na hana thamani.
Uhusiano wenye heshima huruhusu tofauti. Wenza hawalazimishani kufanana, bali wanakubaliana kutofautiana bila kuumizana.
Heshima ina maana ya kusikiliza hata pale unapokosa kukubaliana, na kuthamini hisia za mwenzako hata kama huzielewi kikamilifu.
Hii ndiyo sababu uhusiano wenye heshima huwa na mazungumzo ya wazi, migogoro yenye tija, na uponyaji wa kihisia.
Katika ndoa au uhusiano unaotawaliwa na hofu, mmoja anaweza “kutii,” lakini hakuna furaha. Kuna utulivu wa bandia, si amani.
Heshima, kwa upande mwingine, hujenga amani ya kweli kwa sababu kila mmoja anahisi kuonekana, kusikilizwa na kuthaminiwa. Hii huongeza ukaribu, mapenzi na uaminifu kwa muda mrefu.
Katika dunia inayobadilika, ni muhimu kurekebisha mitazamo ya zamani inayohalalisha hofu katika jina la ndoa au uhusiano.
Sayansi ya uhusiano na sauti za waandishi wa kisasa zinatukumbusha ukweli mmoja muhimu: uhusiano wenye afya haujengwi juu ya kuogopana, bali juu ya kuheshimiana.
Hofu inaweza kumfanya mtu akae, lakini heshima humfanya mtu apende kukaa. Hofu hujenga umbali wa kihisia, heshima hujenga ukaribu.
Ndoa au uhusiano unaodumu si ule ambao mmoja anamwogopa mwenzake, bali ule ambao kila mmoja anajisikia salama, anathaminiwa, na anaheshimiwa kama binadamu kamili.
Kwa kuchagua heshima badala ya hofu, wenza hujenga si tu uhusiano wa kudumu, bali pia maisha ya pamoja yenye furaha, utu na amani ya ndani.
Huo ndio msingi wa mapenzi ya kweli, na huo ndio mwelekeo unaothibitishwa na sayansi, uzoefu na hekima ya waandishi waliotafiti kwa kina uhusiano wa binadamu.