Ingawa inaweza kuonekana kama jambo la ajabu, siku hizi kumeibuka mtindo mpya wa baadhi ya watu kusherehekea talaka.
Kwa kizazi cha zamani, jambo hili ni geni na linakinzana na maadili ya kijamii. Licha ya kuwa linaanza kuzoeleka kutokana na ushawishi wa mitandao ya kijamii, swali la msingi linabaki: Je, kiakili na kiuhalisia, kuna chochote cha kushangilia katika talaka?
Kwa wengi, hasa wale waliofunga ndoa katika misingi isiyoruhusu utengano wa kiholela, talaka haishangiliwi.
Badala yake, huchukuliwa kama msiba na pigo kubwa. Ni vigumu kutoa jibu la moja kwa moja kuhusu kinachowasukuma watu kusherehekea kuvunjika kwa ndoa zao, kwani sababu hutofautiana kulingana na utamaduni na malengo ya wahusika.
Wataalamu wa masuala ya kijamii wanahoji: Je, wahusika wanatafuta umaarufu (kiki), au ni namna ya kujiliwaza na kukomoana?
Katika chapisho la Waite na wenzake (2002), “Does Divorce Make People Happy?”, walibaini kuwa kile kinachoonekana kama “furaha ya kuachika” si furaha halisi, bali ni hisia ya unafuu inayotokana na kulinganisha mateso aliyoyapata mhusika ndani ya ndoa na hali ya kuwa nje ya ndoa hiyo. Vilevile, Zimmermann na wenzake (2006) katika utafiti wao nchini Ujerumani, walihitimisha kuwa maisha ya ndoa huleta utulivu na kuridhika, huku talaka ikiacha athari hasi za kisaikolojia.
Hata katika dini zinazoruhusu talaka, kitendo hicho bado hakichukuliwi kama jambo la heri. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima, anasema: “Kikawaida ndoa ni jambo la heri na furaha, na talaka ni jambo la huzuni ambalo halitarajiwi.”
Hali hii inazua maswali mengi ya kutafakarisha: Je, ndoa hizi hufungwa kwa malengo fulani ya muda mfupi ili zikivunjika wahusika wapate kile walichodhamiria?
Je, ni ndoa za kweli, au ni miungano inayokosa maandalizi ambapo wahusika huishia kuona talaka kama “ukombozi” kutoka kwenye kifungo walichojitakia?Hivi karibuni, kuliripotiwa tukio la mwanamke mmoja nchini aliyealika watu kusherehekea kuvunjika kwa ndoa yake ya tatu. Tukio hili linazua mashaka kuhusu dhamira ya wahusika na afya ya akili katika kufanya uamuzi wa aina hiyo.
Tafakari mfano huu: Ukitaarifiwa msiba wa jirani yako, kisha ukafika na kukuta sherehe badala ya matanga, utajenga dhana gani? Je, binadamu tumeanza kubadilika kiasi cha kushangilia majanga?
Ni vigumu kubaini msukumo wa sherehe hizi, lakini mara nyingi huchochewa na hamu ya kupata wafuasi mitandaoni (kama ilivyo kwa baadhi ya watumiaji wa TikTok) au kutaka kumuumiza mwenza wa zamani.
Inashangaza kuona kuwa mwenendo huu unashika kasi zaidi miongoni mwa wanawake. Hadi sasa, ni nadra kusikia sherehe ya aina hii ikiandaliwa na mwanamume.
Ingawa bado ni mapema kuhukumu utamaduni huu, ni wazi kuwa kuna tatizo fiche ndani ya jamii yetu. Kama jamii, ni lazima tuikabili changamoto hii ili kulinda taasisi ya ndoa isisambaratishwe na ajenda za watu wachache. Si jambo la kawaida kwa binadamu kupata hasara na kisha kusherehekea.
Dk Gwajima ametoa ushauri kwa wataalamu wa saikolojia, uhusiano, na migogoro kufanya utafiti wa kina juu ya jambo hili. Lengo ni kuepuka kuwapotosha vijana ambao wanaweza kuingia kwenye ndoa kwa misingi isiyo imara.
Bila ndoa madhubuti, tunatengeneza taifa lililo hatarini, kwani familia ndiyo msingi wa taifa lolote.
Baadhi ya mambo yanahitaji tafakari ya kina badala ya kufuata mikumbo ya mitandao. Talaka ni jeraha; na jeraha halitibiwi kwa kelele za shamrashamra, bali kwa toba, uponyaji, na kurekebisha makosa.