Katika miaka ya hivi karibuni, malezi ya watoto yameendelea kukabiliwa na changamoto mpya zinazotokana na mabadiliko ya kijamii, kiteknolojia na kiutamaduni.
Miongoni mwa mambo yaliyoathirika kwa kiasi kikubwa ni kupotea kwa utamaduni wa simulizi za hadithi, ambao kwa vizazi vingi ulikuwa nguzo muhimu ya malezi, maadili na malezi ya kisaikolojia ya mtoto.
Wataalamu wa malezi na saikolojia ya watoto wanaeleza kuwa kurejesha utamaduni huu. kunaweza kuwa suluhisho muhimu katika kuboresha mwenendo, mawasiliano na maadili ya kizazi cha sasa.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa saikolojia ya watoto, Dk Janeth Ulimboka, simulizi za hadithi zilikuwa darasa lisilo na ukuta ambalo lililomlea mtoto kwa upole lakini kwa ufanisi mkubwa.
“Kupitia hadithi, mtoto alijifunza mema na mabaya, uvumilivu, bidii, heshima na matokeo ya maamuzi. Mafunzo haya yalimfanya mtoto ajitambue na aelewe mambo mengi sana ya maisha bila kushinikizwa,” anasema Dk Ulimboka.
Kauli ya Dk Ulimboka imenikumbusha jambo, hata wakati mimi nakua, nakumbuka hadithi zilikuwa njia ya kutukumbusha kuishi kwa kuzingatia maadili kwa lugha iliyokuwa inaeleweka kirahisi kwa watoto.
Hivyo, kuporomoka kwa utamaduni wa hadithi kunahusishwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya watu na teknolojia.
Hivi sasa watoto wengi hukulia katika mazingira ya runinga, simu janja na mitandao ya kijamii, ambavyo mara nyingi huwasilisha maudhui yasiyochujwa au yasiyolingana na maadili.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa malezi na elimu ya awali, Profesa Hamisi Khatibu, teknolojia si tatizo, bali tatizo ni pale inapochukua nafasi ya mazungumzo ya ana kwa ana kati ya mzazi na mtoto. Hadithi zilikuwa daraja la mawasiliano na mafunzo ya maisha.
Anasema utamaduni wa simulizi haukuwa tu chombo cha kufundishia maadili, bali pia uliimarisha uhusiano kati ya watoto na wazazi au walezi.
Mtaalamu wa malezi ya familia, Rehema Khamis anafafanua kuwa wakati wa hadithi, ulikuwa pia muda wa familia kukaa pamoja na kusemezana kwa karibu.
“Mzazi alipokuwa akisimulia hadithi, mtoto alihisi kusikilizwa, kuthaminiwa na kupendwa. Huu ulikuwa wakati wa kujenga imani na ukaribu wa kihisia,” anasema.
Ukichambua haya wayasemayo wataalamu, utabaini kwamba kukosekana kwa mawasiliano haya leo, kunachangia watoto wengi kukosa mwongozo wa kihisia na maadili.
Zaidi ya hilo, hadithi zilikuwa njia salama ya kufundisha maadili bila hofu wala vitisho. Kupitia wahusika kama sungura, fisi au simba, watoto walijifunza mambo mengi mazuri ya kuiga katika maisha yao.
Hivyo, wazazi wa sasa wanapaswa kutambua kuwa kuna haja ya kurejesha utamaduni wa kusimuliana hadithi nzuri zenye maadili kwenye familia.
Kwa sababu simulizi za hadithi zilichangia kwa kiasi kikubwa kukuza uwezo wa kufikiri, kusikiliza na kuhoji. Ni wazi kuwa hadithi humsaidia mtoto kukuza ubunifu na uwezo wa kutatua matatizo.
Mtoto anapomsikiliza mhusika wa hadithi akikabiliana na changamoto, hujifunza kufikiri mbadala na kutambua kuwa matatizo yana suluhisho. Hili ni somo muhimu sana katika maisha.
Kupotea kwa utamaduni huu kunajidhihirisha katika mwenendo wa watoto wengi wanaokosa subira, heshima na uwezo wa kudhibiti hisia.
Ndiyo maana wataalamu wa malezi wanaonya kuwa pengo hili lisipozibwa, familia zitaendelea kushuhudia ongezeko la changamoto za kitabia kwa watoto na vijana.
Malezi hayapaswi kuachwa mikononi mwa skrini. Wazazi na walezi wanapaswa kurejesha jukumu lao la pamoja katika kumlea mtoto.
Kurejesha simulizi za hadithi hakuhitaji gharama kubwa wala miundombinu ya kisasa. Kinachohitajika ni dhamira ya wazazi na walezi kutenga muda wa kuzungumza na watoto wao. Hadithi zinaweza kusimuliwa nyumbani au shuleni.
Hata dakika 15 kabla ya kulala zinatosha kusimulia hadithi yenye mafunzo. Kilicho muhimu ni uthabiti na ushiriki wa mzazi.
Kwa ujumla, kurejesha utamaduni wa simulizi za hadithi si suala la kurudi nyuma, bali ni hatua ya makusudi ya kujenga malezi bora yanayoendana na misingi ya utu, maadili na mshikamano.
Katika dunia inayobadilika kwa kasi, hadithi bado zina nafasi muhimu ya kumkuza mtoto aliye kamili kimwili, kiakili na kimaadili.
Familia inayoisimulia hadithi zake, hujenga kizazi kinachoifahamu thamani ya kuwa binadamu.