Nguvu ya maneno chanya inavyogeuza moyo wa mtoto   

Majuzi nilizungumza na Richard anayeishi na mama yake. Baba aliwaacha miaka mingi iliyopita. Richard hajui sababu.

Tangu wakati huo maisha yamekuwa magumu sana. Mama alilazimika kufanya kazi mbili kwa wakati mmoja. Asubuhi alikuwa mfanyakazi ndani. Jioni aligeukia kuuza chakula barabarani.

Hata hivyo, pamoja na jitihada zote hizo maisha yalikuwa magumu. Kila mara alilalamika. Richard alijisikia kusimangwa.

“Mwalimu, kwetu hakuna mtu anayeweza kunielewa. Nimekuwa mzigo tu kwa mama. Hanitaki. Kila anaporudi usiku ni maswali tu yasiyo na mwisho na malalamiko. Sijawahi kusikia maneno kama ‘najivunia kuwa mama yako’ au hata ‘asante kwa kazi nzuri uliyoifanya’. Najiona kama msumbufu tu.”

Richard, kwa sasa, amejitenga kabisa na familia. Muda mwingi anakuwa anazurura mtaani. Huko ndiko anakutana na marafiki wasio na ushawishi mzuri. Richard akaanza kunywa pombe. Richard akaanza kuvuta sigara. Shuleni alianza kuzorota. Richard akawa mtoro. Ufaulu wake ulianza kushuka. Walimu walimpachika jina jipya, “haambiliki”, “mtoto kichwa ngumu”, “asiye na nidhamu”.

Richard, kwa kumsikiliza na kumwelewa, alikuwa kapoteza kabisa utambulisho wake wa kujipenda. Hakujua tena yeye ni nani hasa, wala hakujua ikiwa kuna mtu anayeweza kumthamini kwa dhati.

Maswali yaleyale yanayowasumbua vijana wengi katika umri wa uchanga yalikuwa yakimtesa kila siku: “Mimi ni nani hasa? Je, nina thamani gani hapa duniani? Kuna kitu gani kizuri ndani yangu ambacho kingenifanya nihitajike na watu?”

Mazungumzo yangu na Richard yalianza hatua kwa hatua. Mahali pa kuanzia nikaona ni kujenga uaminifu. “Unapenda kufanya nini ukiwa peke yako?”

“Hakuna” alijibu kirahisi. Tungeweza kuzungumza muda mrefu na majibu yake yakiwa yamefungwa na sentensi zile zile za “Sipendwi”, “Siaminiki”, “Sithaminiki.” Sikukata tamaa. Baada ya wiki kadhaa za mazungumzo ya mara kwa mara, Richard alianza kufunguka kidogo kidogo.

“Napenda kuchora.” Ilikuwa hatua kubwa. Kesho yake alibeba daftari lake la michoro kunionesha. Richard alikuwa na kipaji cha aina yake.

Ukichunguza michoro yake unakutana na hisia nyingi sana. Richard alitumia michoro kuonesha maumivu yake, hasira yake, na hata matumaini yaliyofichika.

“Richard, umetisha sana. Sikujua wewe msanii mkali wa kiwango hiki.”Uso wake ulianza kupata nuru. “Michoro inazungumza mambo makubwa sana. Una kipawa ambacho vijana wengi wa umri wako hawana.”

Tabasamu likaufunika uso wa Richard.

“Una uwezo wa kuonyesha hisia zako kwa njia ambayo maneno matupu hayawezi.” Richard akanitazama kwa mshangao. Ni wazi hakutarajia kusikia maneno kama hayo.

Nilimpa zoezi dogo. “Nenda kaandike na ukiweza chora kitu kimoja tu unachokipenda kuhusu wewe mwenyewe.”

“Siwezi” alisema. “Najua hujawahi kujaribu. Ukijaribu utaweza.” Richard akanijia na picha za ajabu sana. Tukazizungumzia. Richard akaanza kufurahia mazungumzo yetu.

Nikaamua kumwalika mama kwenye kikao cha pamoja. Mama alikuja akiwa kajaa wasiwasi mkubwa. Huenda alidhani nilimwita kwa sababu Richard ameingia matatizoni. Uso wake ulionyesha uchovu mwingi.

Ilibidi niweke wazi, “Leo hatuzungumzii makosa yoyote ya Richard. Tunazungumzia sifa nzuri alizonazo.”

“Sifa zipi kwa huyu?” Hakuwa anaamini kuna chochote chema cha kujadili kumhusu Richard. Nilimshawishi. Hatimaye akakubali. Nikampa karatasi na kalamu. Kazi yako sasa ni kuorodhesha sifa kumi nzuri unazozijua kwa Richard.

Mama alitulia tuli kwa muda mrefu sana. Machozi yalianza kumlenga lenga. Kazi haikuwa rahisi. “Sijawahi kufikiria Richard angekuwa na sifa nzuri hata kidogo. Namwona kama mtoto anayenipasua kichwa. Sijui kama ninaweza.” Baada ya muda, alianza kuandika polepole. Kidogo nikaona akicheka mwenyewe.

Tulipompa Richard karatasi aisome mwenyewe, alibaki kimya kwa muda mrefu. Machozi yakamdondoka. Huenda hakuamini alichokuwa anakosoma.

“Una upole fulani kazuri… unapenda kusaidia wengine bila kuulizwa hata kama huambiwi… una akili ya haraka unapoelewa kitu… una kipaji cha kuchora vizuri sana… nafurahi unavyopambana na maisha magumu bila kulalamika kila wakati.”

 “Mama, umeandika hivi kweli? Unamaanisha?” Mama akamuwahi na kumkumbatia kwa nguvu kubwa. “Ndiyo, mwanangu. Nisamehe kwa kwa kutokuambia haya mapema. Mara zote nimekuwa mtu wa kuangalia makosa yako tu. Leo nimekuona kwa jicho jingine.”

Kufupisha habari, Richard alianza kubadilika kidogo kidogo. Richard alianza kurudi nyumbani mapema zaidi badala ya kuzurura mitaani usiku. Richard alianza kuonyesha michoro yake mpya kwa mama yake na kumuuliza maoni yake.

Mama alianza kujifunza kumsifia na kumshukuru kwa kila mabadiliko madogo aliyoona. Richard alianza kutia bidii masomoni. Miezi michache baadaye, Richard alinifuata, “Mwalimu, sasa najisikia mtu. Sijawahi kujisikia hivi tangu niwe na akili.

Maneno chanya yanapotoka kwa watu wa karibu zaidi, hasa mzazi au mlezi, yana nguvu ya kipekee ya kurekebisha moyo wa mtoto uliochoka. Hata kama umechelewa miaka mingi, bado unaweza kuanza leo.