INAELEZWA Alliance Girls ya Mwanza imekamilisha usajili wa wachezaji watatu waliokuwepo kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa yaliyofanyika jijini Mwanza.
Alliance iko nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikikusanya pointi 20 kwenye mechi tisa imeshinda sita, sare moja na kupoteza mechi mbili.
Wachezaji hao ni Hafsa Baruani kutoka Mshikamano Queens ambaye kwenye mashindano hayo alikuwa na Simbas Footprint ya Tanga, Dativa Karitus aliyekuwa na kikosi cha Victoria Women na Jelly Joab kutoka Mpaju Queens ya Mbeya.
Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo imeeleza kuwa sababu ya kuwasajili nyota hao ni kutengeneza kizazi cha nyota wachanga ambao anaamini kutokana na vipaji vyao wanaweza kuwa na msaada baadae.
Iliongeza maeneo mengine ambayo atayafanyia kazi kwenye ushambuliaji bado timu hiyo haina safu nzuri ya kushambulia na kwenye mechi 10 imefunga mabao tisa na kuruhusu nane.
“Ni wachezaji ambao bado hawana uzoefu lakini wana vipaji vikubwa lengo letu ni kuendeleza kile walichokuwa nacho, hivyo ligi kuu inaweza kuwa sehemu yao ya kujitangaza na kukuza karia zao.”