Mwinyi Zahera aanza visingizio WPL

KOCHA wa Ruangwa Queens, Mwinyi Zahera ametaja sababu ya kutoanza vizuri Ligi ya Wanawake ni pamoja na wachezaji kutokuwa na uzoefu wa kimashindano.

Amesema ingawa wamesajili wachezaji 26, wengi wao hawajawahi kucheza Ligi Kuu, jambo ambalo limeathiri wanapokutana na timu ngumu kama JKT Queens na Simba Queens.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwinyi amesema kutokana na changamoto hiyo timu iko kwenye msako wa kutafuta washambuliaji wanne dirisha hilo la usajili ambao watakuwa na kasi na nguvu, ili kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji. Lengo ni kuhakikisha timu inapata mabao zaidi na kuboresha matokeo yaliyokua mabaya mwanzoni mwa msimu.

Aliongeza, kati ya wachezaji waliosajiliwa, saba wamepandishwa timu ya vijana huku wengine wakiwa bado wanahitaji muda wa kuzoea mfumo wa timu.

“Hatuna muda mrefu kwenye ligi, ndio kwanza tunacheza msimu wetu wa kwanza, timu zimejipanga sana ndani na nje ya uwanja na sababu nyingine inayotufanya tupoteze ni mambo pia ya nje, timu zinapambana sana nje kuliko uwanjani,” amesema Mwinyi na kuongeza

Kocha huyo wa zamani wa Yanga aliongeza “Hivyo tunahitaji kuongeza wachezaji wenye kasi na nguvu katika safu ya mbele kwa sababu safu ya ulinzi haina shida tunaamini tukifanikisha hilo inaweza ksuaidia kwa sababu bado ligi inaendelea.”