Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Bukoba imeruhusu Karagwe Development Association (Karadea), mmiliki wa Shule ya Msingi Omukarilo, kujitetea katika kesi ya madai ya michango ya zaidi ya Sh127 milioni anayodaiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Uamuzi huo ulitolewa Januari 22, 2026 na Jaji Immaculata Banz, aliyekuwa akisikiliza maombi ya madai namba 28301 yaliyotokana na kesi ya msingi ya madai namba 22670 ya mwaka 2025. Nakala ya uamuzi huo imewekwa kwenye tovuti ya Mahakama.
Kupitia maombi hayo, Karadea kwa niaba ya shule hiyo iliwasilisha shauri dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Bodi ya Wadhamini wa NSSF.
Awali, Agosti 2025, wadaiwa waliwasilisha kesi ya madai wakidai zaidi ya Sh64.8 milioni ikiwa ni michango mikuu ya wanachama kwa kipindi cha Januari 2019 hadi Oktoba 2023, pamoja na zaidi ya Sh62.4 milioni kama adhabu ya kuchelewa kulipa michango hiyo.
Baada ya kuwasilishwa kwa kesi hiyo, mwombaji aliomba ruhusa ya kushiriki katika kesi ya msingi na kujitetea dhidi ya madai yanayomkabili. Ombi hilo liliungwa mkono na hati ya kiapo ya Ofisa Mkuu wa Karadea, Ditrick Ernest.
Wakati wa usikilizwaji wa awali wa maombi hayo, wadaiwa wakiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Nestory Lutambi walikubali ombi hilo kwa sharti kwamba mwombaji aweke fedha taslimu au dhamana isiyopungua asilimia 50 ya kiasi cha michango inayodaiwa.
Kwa mujibu wa amri ya Mahakama, Desemba 19, 2025, mwombaji aliwasilisha dhamana kwa kuweka hati yake ya awali ya umiliki wa ardhi namba 57KGW/2380 chini ya hati ya kimila, anayomiliki eneo lenye ukubwa wa ekari 49.658 lililopo Kijiji cha Chabukora, wilayani Karagwe.
Eneo hilo lina thamani ya Sh130 milioni kwa mujibu wa ripoti ya uthamini ya Januari 14, 2026.
Akitoa uamuzi wake, Jaji Banzi amesema Mahakama imechunguza kwa kina hati ya kiapo ya mwombaji pamoja na viambatisho vyake na kubaini kuwepo kwa masuala yenye utata kuhusu usahihi wa madai yaliyowasilishwa na NSSF.
Alieleza kuwa nyaraka zilizotolewa na NSSF zinaonesha tofauti katika vipindi vya madeni yanayodaiwa, pamoja na kujumuisha majina ya watu ambao kwa mujibu wa mwombaji, hawakuwa wafanyakazi wake tangu mwaka 2019, huku baadhi yao wakidaiwa kuwa tayari walishalipwa mafao yao.
Jaji Banzi amesema Mahakama pia imezingatia hoja ya mwombaji kuwa alilipa kikamilifu michango ya wanachama wake kwa kipindi cha mwaka 2019 hadi 2021, madai yaliyothibitishwa kwa kuwasilishwa kwa risiti kama vielelezo.
“Chini ya aya ya 6, 7, 8 na 9 za hati ya kiapo, mwombaji anaeleza kuwa kiambatisho NSSF-2 kina tofauti kubwa katika vipindi vya madeni yanayodaiwa, kwa kuwa kinajumuisha majina ya watu ambao hawakuwa wafanyakazi wake tangu mwaka 2019 na baadhi yao walishalipwa marupurupu yao na mjibu maombi wa pili,” amesema Jaji.
Ameongeza kuwa, “Kwa kuzingatia hoja zilizowasilishwa katika hati ya kiapo, ni dhahiri kuwa kuna suala lenye utata kuhusu michango inayodaiwa. Hivyo, ninakubali ombi hili na kumpa mwombaji ruhusa ya kujitokeza na kujitetea katika kesi ya madai namba 22670 ya mwaka 2025.”
Uamuzi huo umefungua mlango wa kusikilizwa kwa kesi ya msingi, pande zote zitapata fursa ya kuwasilisha ushahidi na hoja zao ili kubaini uhalali wa madai ya michango pamoja na adhabu zinazodaiwa na NSSF.