Unguja. Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla, amesema Mahakama ya Zanzibar inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha na kukuza usawa wa kijinsia ndani ya mfumo wa utoaji haki, ikiwa ni sehemu ya mageuzi ya kiutendaji yanayolenga kuhakikisha haki inapatikana kwa usawa kwa makundi yote ya jamii.
Kauli hiyo ameitoa leo, Jumapili, Januari 25, 2026, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Mkakati wa Haki za Kijinsia kwa kipindi cha mwaka 2026 hadi 2030, mkakati unaolenga kujenga mfumo wa haki unaozingatia misingi ya usawa, ujumuishi na unaojali mahitaji ya jinsia zote.
Jaji Khamis amesema Mahakama inatambua changamoto mbalimbali za kijinsia zilizopo katika jamii na namna zinavyoathiri upatikanaji wa haki, hususan kwa wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu.
Amesema hali hiyo imeilazimu Mahakama kuweka mkazo katika kujenga taasisi inayozingatia misingi ya usawa, uwajibikaji na haki kwa wote bila ubaguzi.
“Mahakama inatambua changamoto za kijinsia zilizopo katika jamii na athari zake katika upatikanaji wa haki, hivyo ni dhamira yetu kuendelea kujenga taasisi jumuishi inayozingatia misingi ya haki na usawa kwa wananchi wote,” amesema Jaji Khamis.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu huyo, mkakati wa haki za kijinsia umeandaliwa kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi ndani ya Mahakama, kuongeza ushiriki wa kijinsia katika nafasi za uongozi, pamoja na kuhakikisha huduma za kimahakama zinatolewa kwa kuzingatia mahitaji ya jinsia zote bila ubaguzi wa aina yoyote.
Amesema utekelezaji wa mkakati huo utahusisha utoaji wa mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi wa Mahakama ili kuwaongezea uelewa kuhusu masuala ya kijinsia, kufanya maboresho ya sera na taratibu za ndani, pamoja na kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali wa haki nchini ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Jaji Khamis amesema Mahakama itaendelea kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa mkakati wa haki za kijinsia ili kuhakikisha unaleta matokeo chanya katika utoaji wa haki, pamoja na kuimarisha imani ya wananchi kwa mhimili wa Mahakama.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mratibu wa Mradi wa Maboresho ya Mahakama Zanzibar (Zi-JUMP), Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim, amesema Mahakama imeanza utekelezaji wa mafunzo ya awali ya mkakati wa haki za kijinsia kwa wakuu wa taasisi zinazosimamia haki, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usawa wa kijinsia katika mfumo wa utoaji haki.
Amesema mafunzo hayo yatafanyika kwa awamu tatu zitakazohusisha wakuu wa taasisi, mahakimu na makadhi, pamoja na wafanyakazi wa kawaida wa Mahakama, ili kuhakikisha mkakati huo unafahamika na kutekelezwa kwa ufanisi katika ngazi zote.
Jaji Ibrahim amebainisha kuwa mafunzo hayo yanatoa fursa kwa washiriki kutoa maoni, mapendekezo na michango yao kuhusu mkakati uliowasilishwa, kwa lengo la kuuboresha zaidi kabla ya kuanza kutumika rasmi, ili hatimaye kupata mkakati wenye ubora unaokidhi viwango vya kimataifa.
Kwa upande wake, mwezeshaji wa mafunzo ya Mkakati wa Haki za Kijinsia, Carsten Mahnke kutoka Ujerumani, amepongeza uongozi wa Mahakama ya Zanzibar kwa kumuamini na kumpa fursa ya kuwasilisha mafunzo hayo.
Pia amewashukuru wadau wote, wakiwemo taasisi za Serikali, sekta binafsi na wananchi, kwa mchango wao katika ukusanyaji wa taarifa zilizotumika kuandaa mkakati huo.
Amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kubadilishana mawazo, uzoefu na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuandaa mkakati bora, jumuishi na unaoendana na mahitaji halisi ya taasisi za haki na jamii kwa ujumla.