KVZ yabeba taji netiboli, Masauni akitia neno

MAAFANDE wa KVZ ya visiwani hapa imebeba ubingwa wa Ligi ya Muungano kwa mchezo wa netiboli, huku Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Injini Hamad Masauni akisema Maendeleo ya michezo yamechangiwa na juhudi kubwa za viongozi wakuu wa nchi waliotoa kipaumbele katika sekta hiyo.

Katika michuano hiyo iliyoshirikisha jumla ya timu 11, zikiwamo tano za Zanzibar na sita kutoka Bara, KVZ iliibuka mabingwa baada ya kushinda michezo yote 10 na kuzipiku timu nyingine na kukabidhiwa taji hilo la Waziri Masauni aliyekuwa mgeni rasmi wa hafla ya ufungwaji wa michuano hiyo.

Waziri Masauni amesema uwezekaji katika michezo ni chachu kubwa ya maendeleo na kusema kama taifa limepiga hatua kutokana na viongozi wakuu wa Tanzania, akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan na Dk Hussein Ali Mwinyi kuweka kipaumbele kikubwa katika sekta hiyo.

KV 01


“Kupitia mpango wa ‘Goli la Mama’, tumeshuhudia ongezeko la bajeti, ujenzi wa viwanja vipya na mazingira bora kwa wanamichezo wetu, matokeo ya jitihada hizi ni wazi na tumeshuhudia timu ya taifa ya soka, Taifa Stars imefika hadi hatua ya 16 bora ya michuano ya AFCON 2025 pale Morocco na ni kwa mara ya kwanza tangu kuanza kushiriki mashindano hayo,” amesema Masauni.

Aliongeza ujenzi pamoja na uboreshaji wa viwanja vya michezo vimewezesha mashindano mbalimbali kufanyika yakiwemo ya CHAN yaliyoandaliwa kwa pamoja na nchi za Kenya, Uganda na Tanzania.

KV 02


Huu ni ushahidi Tanzania kupitia Muungano wake, inainuka kisoka Afrika na duniani.

Amesema maendeleo haya yamewekewa chachu ya ushirikiano kati ya serikali zetu mbili chini ya wizara husika za michezo na taasisi zetu za ZFF, TFF, CHANEZA na CHANETA ambazo zinasimamia michezo ya soka na netiboli kwa  weledi mkubwa.

“Nawapongeza viongozi wa wizara hizi na wasaidizi wao pamoja na viongozi wa mashirikisho na vyama vinavyosimamia michezo hiyo kwa kuhakikisha wanasimamia maendeleo ya michezo nchini,” amesema Masauni, huku akiwapongeza na kuwashukuru waandaaji wa michuano hiyo ya Ligi ya Muungano ya Netiboli.

KV 03


Kwa upande wa Mwenyekiti wa CHANEZA, Nasra Juma ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushiriki na kudhamini mashindano hayo ambayo yamekuwa ya ushindani mkubwa.

Amesema mashindano hayo ni muhimu kwa kuwa yamekuwa yakitoa wawakilishi wa Tanzania katika mashindano makubwa kwa Bara la Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki.