Moshi. Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Moshi Vijijini, umewataka vijana kuwa mstari wa mbele katika kulinda taswira, heshima na masilahi ya Taifa kwa kuzingatia maadili na uzalendo, hususan kupitia matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii.
Rai hiyo imetolewa leo Januari 25 na Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Yuvenal Shirima, wakati akitoa maazimio ya kikao cha baraza la umoja huo kilichofanyika wilayani humo, akisisitiza kuwa vijana wana wajibu mkubwa wa kulinda amani, kuimarisha mshikamano na kuchangia maendeleo ya Taifa.
“Baraza tumeazimia kulinda taswira, heshima na uzalendo wa Taifa letu, hususan katika matumizi ya mitandao ya kijamii, vyombo vya habari na majukwaa ya umma, kwa kuzingatia maadili, mshikamano na uzalendo wa Taifa,” amesema Shirima.
Ameeleza kuwa taswira bora ya Taifa ni msingi wa kuaminika, kuungwa mkono na kushirikishwa katika maendeleo ya kitaifa na kimataifa, huku akisisitiza kuwa vijana wanapaswa kuchukua nafasi ya mstari wa mbele katika kulinda heshima ya nchi, kuimarisha mshikamano wa wananchi na kuchochea maendeleo endelevu.
Aidha, Shirima amesema Baraza hilo pia limeazimia kusimamia nidhamu, maadili, mshikamano na uwajibikaji wa viongozi wa UVCCM katika ngazi zote za wilaya, ili kuhakikisha unazingatia misingi ya haki, sheria na masilahi ya vijana.
Mwenyekiti wa Umoja wa vijana wa chama cha Mapinduzi (UVCCM), Wilaya ya Moshi Vijijini, Yuvenal Shirima, akizungumza wakati akitoa maazimio ya kikao cha Baraza la Umoja huo kilichofanyika wilayani humo. Picha na Janeth Joseph
“Hatutomfumbia macho kiongozi au mtu yeyote atakayejihusisha na vitendo vya kuvuruga masilahi ya vijana, kukiuka sheria, taratibu au maadili ya chama na Taifa. Baraza linatoa onyo kali kuwa yeyote atakayejihusisha na tabia za ubinafsi, uchochezi au kuvuruga mshikamano atachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi,” amesema.
Baraza hilo pia limeeleza masikitiko yake juu ya mienendo ya baadhi ya watu wanaotumia nafasi zao katika jamii kueneza kauli za uchochezi, migawanyiko, vurugu na maandamano yasiyo na tija, hatua zinazohatarisha amani na utulivu wa Taifa.
Katika hatua nyingine, Shirima ametoa wito kwa viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani, upendo na mshikamano, akisisitiza kuwa dini ni nguzo muhimu ya maadili na amani, na si chombo cha kuchochea migawanyiko ndani ya jamii.
Vilevile, amewataka wazee waliostaafu katika nyanja mbalimbali za uongozi kutumia uzoefu wao kuijenga jamii na kuwa washauri wa kizalendo kwa vijana, badala ya kuwa sehemu ya kubeza, kuchochea taharuki au kuvuruga mwelekeo wa Taifa.
Baraza hilo pia limempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ya maendeleo anayoifanya nchini, likisisitiza kuwa UVCCM itaendelea kumuunga mkono kwa kuhamasisha uzalendo, mshikamano na ushiriki wa vijana katika maendeleo ya wilaya na Taifa kwa ujumla.
Naye, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Same, Azza Karisha, ameipongeza Serikali ya awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha wizara ya vijana, akisema itawasaidia kujishughulisha na kuchangamkia fursa zinazojitokeza zaidi ya kukesha kwenye mitandao na kulalamika.