Waziri Dk Gwajima awatumia salamu wanaokwamisha huduma za wenye uhitaji

Dodoma. Waziri wa Maendeleo ya Jamii Wanawake,Jinsia na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima amesema wanaokwamisha utekelezaji wa majukumu, hatawavumilia.

Hata amesema mpango wa baadaye ni kuhakikisha kunakuwa na mafunzo maalumu kwa mabinti na vijana ya jinsi ya kuwalea watoto na watakaopitia mfumo huo watarasimishwa pia.

Dk Gwajima ametoa kauli hiyo leo Jumapili Januari 25,2026 wakati akitoa ufafanuzi wa utekelezaji wa ahadi za Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya siku 100.

“Nilifanya ziara yangu pale Ubungo nikakuta kuna baadhi ya mambo yanakwenda ndivyo sivyo, tulitatua palepale na huduma zikatokea, nawatumia taarifa watendaji ngazi ya chini tutawafuata na kushughulika nao,” amesema Dk Gwajima.

Amesema ndani ya siku 100 wamepata mafanikio ikiwemo  usajili wa wafanyabiashara ndogondogo 19,595 na katika kipindi hicho wamepokea jumla ya Sh1.5 bilioni kwa ajili ya kutoa mikopo yenye riba nafuu ya asilimia saba.

Hata hivyo katika orodha ya waliosajiliwa na kupewa vitambulisho vya kidijitali, idadi ya waendesha bodaboda imeonekana kuwa ndogo kwani waliosajiliwa kwenye mfumo huo wapo 4,109 ingawa  amesema usajili ni hiari.

Akielezea mkakati wa baadaye,   Dk Gwajima amesema Serikali inakuja na mkakati wa kufundisha wafanyakazi wa ndani hasa wanaohudumia watoto ili wale wenye uhitaji waweze kupatiwa watu ambao wana sifa kupitia kwa maofisa ustawi wa jamii.

“Mkakati huu utasaidia mabinti na vijana wanaofanya kazi za ndani nao kurasimishwa ili wajue namna bora ya kuwalea watoto na kuwapa lishe, siyo uji wa ukwaju bora alale, haiwezekani,” amesema Dk Gwajima.

Ameeleza kuwa, alitembelea kwenye mataifa mbalimbali na kujionea namna wanavyoweza kuwalea watoto kwa kuangalia mahitaji ya baadaye, ili mtoto akikua hashangai kila anachokiona kwani alishaanza kuwa nacho tangu utoto.