Maswa. Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (Mauwasa) imewaonya wananchi wanaojiunganishia huduma ya maji kinyume cha sheria kuacha mara moja vitendo hivyo, ikieleza hatua hiyo inasababisha hasara kwa mamlaka hiyo na kuhatarisha upatikanaji wa maji kwa wananchi wengine.
Akizungumza leo Januari 25,2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa, Nandi Mathias amesema wamebaini kuwepo kwa baadhi ya wananchi wanaojiunganishia huduma hiyo kufuata taratibu za kisheria, jambo linalochangia matumizi ya maji bila malipo pamoja na uharibifu wa miundombinu.
Amesema kuwa vitendo vya kuingilia miundombinu ya maji siyo tu vinakiuka sheria ya maji ya mwaka 2019, bali pia vinaweza kusababisha usumbufu wa huduma kwa wananchi wanaolipa kwa uhalali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa, Mhandisi Nandi Mathias, akizungumza na waandishi wa habari juu ya wizi wa maji unaofanywa na wananchi. Picha na Samwel Mwanga
Ametoa mfano wa tukio la Januari 23, 2026 ambapo Mauwasa ilimkamata mwananchi aitwaye Esther Daud, mkazi wa Uzunguni mjini Maswa, akitumia maji ambayo hayakuwa yakipitia kwenye mita kwa kipindi cha miezi minne.
“Esther Daud alikuwa anatumia akaunti ya maji ya Ladislaus Kiatu, mkazi wa Uzunguni. Huduma yake ilisimamishwa kutokana na kushindwa kulipa bili ya maji, lakini tumemkamata akijiunganishia maji kinyume cha sheria. Tayari tumemkabidhi kwa vyombo vya sheria ili hatua za kisheria zichukuliwe,” amesema.
Ameongeza kuwa mamlaka hiyo inaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa watumiaji wote wa huduma zake kama sehemu ya jitihada za kudhibiti wizi wa maji na uharibifu wa miundombinu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Uzunguni mjini Maswa, Caroline Shayo, amelaani vikali vitendo vya wizi wa maji amesema kuwa ni sawa na uhujumu wa uchumi na vinachangia kurudisha nyuma maendeleo ya jamii.
“Nilishuhudia tukio hilo na ni kweli kabisa. Wizi wa maji ni sawa na kuhujumu mali ya umma. Maji ni rasilimali ya wote, hivyo yeyote anayeyaiba anawanyima wengine haki yao,” amesema.
Sehemu ya jengo la Ofisi za Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa (Mauwasa). Picha na Samwel Mwanga
Naye Getruda John mkazi wa mjini Maswa amesema kuwa anaunga mkono hatua zinazochukuliwa na Mauwasa huku akitaka sheria isimamiwe bila muhali.
“Tunaojiunganishia kihalali tunapata shida kubwa. Maji yanapungua au kukatika kwa sababu kuna watu wanajiunganishia kwa siri,” amesema.
Severine Mutegeki amesema ni muhimu kwa Mauwasa kuendelea na ukaguzi wa mara kwa mara.
“Hatua hii ni nzuri. Inapaswa kuendelea ili kulinda mapato ya mamlaka na kuhakikisha maji yanawafikia wananchi kwa usawa,” amesema.