Arusha. Wakulima nchini wanatarajiwa kuanza kunufaika na matumizi ya mwanga wa jua katika kuendesha shughuli zao za kilimo baada ya Chama cha Wakulima Tanganyika (TFA), kusaini mkataba wa makubaliano ya kutoa huduma hiyo na kampuni ya teknolojia ya nishati ya Zola.
Lengo kubwa la mkataba huo ni kutoa elimu ya matumizi ya nishati ya jua lakini pia kuwezesha usimikaji wa vifaa vya kusaidia uvunaji wa nishati hiyo kwa matumizi mbalimbali ya nyumbani na shambani.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TFA, Justin Shirima, amesema kupitia mkataba huo, wakulima watawezeshwa kupata huduma za nishati ya sola kwa mfumo wa ukopeshaji, ambapo watalipa kidogokidogo kuanzia Sh500 kwa siku.
Amesema lengo ni kuimarisha kilimo cha kisasa hususan maeneo ya vijijini na kuwafanya wakulima wengi zaidi kumudu teknolojia hiyo bila mzigo mkubwa wa kifedha
“Tunalenga kuwapa elimu wakulima wakiwemo wanachama wetu zaidi ya 5,000 juu ya matumizi ya nishati ya sola katika utatuzi wa changamoto za uzalishaji hasa kilimo.”
Amesema wataelimisha wakulima kutumia nishati ya umeme wa jua katika uendeshaji wa mashamba ikiwemo umwagiliaji, uhifadhi wa mbegu na dawa katika majokofu na uhifadhi wa mazao baada ya mavuno.
Shirima amesema wakulima wengi walioko vijijini ambao ni wanachama wao na wadau muhimu wa sekta ya kilimo, lakini bado hawana elimu ya kilimo cha kisasa wala matumizi ya teknolojia hivyo watahakikisha wanafikiwa na fursa hiyo na masilahi yao yanaunganishwa moja kwa moja na maendeleo ya teknolojia ya nishati.
Mkurugenzi wa Zola, Johnson Kiwanko, amesema kampuni hiyo ya kiteknolojia inayotumia akili mnemba (AI) katika utoaji wa huduma za nishati, imeona uhitaji mkubwa wa nishati ya sola kwa wakulima nchini ndio maana wameamua kuingia mkataba huo.
Amesema kampuni hiyo ya kwanza duniani kutumia teknolojia hiyo katika sekta ya nishati itawezesha wanachama wa TFA na wakulima wengine kupata si tu uelewa wa teknolojia hiyo, bali pia huduma za nishati safi zitakazosaidia kuboresha maisha yao na kuendeleza kilimo chenye tija.
“Mkataba huu ni wa muda mrefu na kila mwaka tutakuwa tukikutana kutathmini utekelezaji wake na kubaini maeneo ya kuboresha ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia,” amesema Kiwanko.
Mmoja wa wanachama wa TFA, Abel Sirikwa amesema TFA yenye wanachama zaidi ya 5,000 na mtandao wa wateja unaozidi milioni mbili nchi nzima changamoto kubwa kwa sasa ni zana za kilimo zenye kutumia nishati ya jua.