Azam yafanya kweli CAF, Kitambala akiandika rekodi mpya

Mshambuliaji wa Azam, Jephte Kitambala, ameandika rekodi mpya baada ya kuifungia timu hiyo bao la kwanza la michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, kufuatia ushindi wa kikosi hicho wa mabao 2-1, dhidi ya Nairobi United ya Kenya.

Kitambala aliyejiunga na Azam, Agosti 10, 2025, akitokea AS Maniema Union ya kwao DR Congo, amefunga bao hilo likiwa ni la kusawazisha dakika ya 17, baada ya piga nikupige katika lango la timu ya Nairobi akipokea pasi ya beki, Yoro Diaby.

Katika mechi hiyo ya kundi B, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Nyayo Kenya, wenyeji Nairobi ilitangulia kupata bao la kwanza dakika ya 14, lililofungwa na Dancan Odhiambo, aliyeunganisha mpira uliomshinda kipa wa Azam FC, Zuberi Foba.

Hata hivyo, licha ya timu zote kushambuliana kwa zamu, ila Azam iliandika bao la pili dakika ya 78, baada ya kipa wa Nairobi, Ernest Mohammed kujifunga, kufuatia mpira uliopigwa na kiungo, Himid Mao Mkami na kumgusa akiwa katika harakati za kuokoa.

AZA 01


Ushindi huo kwa Azam ni wa kwanza msimu huu katika michuano hiyo, baada ya kuchapwa mechi mbili mfululizo za hatua ya makundi, ikichapwa mabao 2-0, dhidi ya Maniema Union ya DR Congo, kisha kupoteza bao 1-0 na Wydad Casablanca ya Morocco.

Azam FC iliandika historia mpya katika Michuano ya CAF, baada ya timu hiyo kuandika rekodi ya kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa Julai 23, 2004 ikifahamika kwa jina la Mzizima FC.

Matajiri hao wa Jiji la Dar es Salaam, waliopanda rasmi Ligi Kuu Julai 27, 2008, wameweka historia mpya tangu kuanzishwa kwake chini ya Kocha Mkuu, Mkongomani Florent Ibenge aliyejiunga nao Julai 5, 2025, akitokea Al Hilal Omdurman ya Sudan.

AZA 02


Matokeo haya kwa Azam, yanaifanya kushika nafasi ya tatu na pointi tatu, nyuma ya vinara, Wydad Casablanca ya Morocco yenye sita, itakayocheza saa 4:00 usiku huu dhidi ya Maniema Union ya DR Congo iliyo nafasi ya pili na pointi sita pia.

Kwa upande wa Nairobi United iliandika pia historia ya kufuzu kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiing’oa kwa penalti 7-6, mabingwa wa zamani wa CAF, Etoile du Sahel kutoka Tunisia, baada ya sare ya mabao 2-2.

Timu hiyo iliyoanzishwa rasmi mwaka 2015, ikifahamika kwa jina la Balaji EPZ kabla ya kubadilishwa mwaka 2022 na kuitwa Nairobi United, inaburuza mkiani mwa kundi hilo, baada ya kuchapwa pia mechi zote tatu ilizocheza hadi sasa msimu huu.

Nairobi United ilianza hatua ya makundi kwa kuchapwa mabao 3-0 na Wydad Casablanca ya Morocco, ikachapwa tena bao 1-0 na Maniema Union ya DR Congo, kisha 2-1 na Azam FC, ambapo matokeo hayo yanakifanya kikosi hicho kuendelea kuburuza mkiani.

Ushindi kwa Azam unaiweka katika nafasi nzuri ya kusaka tiketi ya kusonga hatua ya robo fainali, ikiwa itashinda mechi ijayo wakati timu hiyo itakapokuwa kwenye Uwanja wa Amaan Complex visiwani Zanzibar kuikaribisha tena Nairobi United.