Kwa Mudrick, haina kupoa Uturuki

BEKI wa Mersin inayoshiriki Ligi Kuu ya Walemavu Uturuki, Mudrick Mohamed amesema ushindani wa namba katika kikosi hicho ni mkubwa lakini ni chachu inayomfanya azidi kupambana kila anapopata nafasi.

Mudrick alipata nafasi ya kusajiliwa kikosini hapo baada ya kuonyesha kiwango bora katika mashindano ya Kombe la Dunia yaliyofanyika Uturuki.

Akizungumzia na Mwanaspoti, Mudrick amesema hakuna nafasi ya kubweteka kutokana na ushindani uliopo akitaja siri ya kuendelea kuaminiwa kikosini hapo ni pamoja na juhudi na kucheza nafasi mbalimbali uwanjani.

“Hapa kila mchezaji anapigania namba ushindani ni mkubwa, lakini unanijenga na kunifanya nifanye kazi kwa bidii zaidi kila siku,” amesema Mudrick na kuongeza;

“Mimi huwa nacheza nafasi tofauti muda mwingine nacheza kiungo kulingana na kocha anavyotaka kuiendea mechi kwahiyo ninapokabidhiwa jukumu la kucheza namba tofauti nafanya kazi kweli kweli.”

Nyota huyo pia alieleza namna ambavyo watanzania wanavyopambania timu wanazocheza kwenye ligi hiyo kubwa na kuendelea kuacha alama kubwa.

“Watanzania tunaiwakilisha nchi vizuri nidhamu, juhudi na kujituma vinatufanya tuheshimiwe kwenye ligi hii kubwa.”