‘Ushindi ni mchakato’. Ni kauli ya Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Zedekiah Otieno akielezea matokeo ya bila kufungana dhidi ya JKT Tanzania na mwenendo wa timu hiyo Ligi Kuu hadi sasa.
Kocha huyo raia wa Kenya, amejiunga na Maafande hao mapema msimu huu, ambapo hawajawa na matokeo mazuri wakiwa nafasi ya 14 kwa pointi 8 baada ya michezo tisa.
Akizungumza leo Januari 25, 2026 baada ya mchezo dhidi ya JKT Tanzania uliopigwa Uwanja wa Sokoine jijini hapa, Otieno amesema suala la ushindi ni mchakato na bado wanayo nafasi ya kubadilika na kufanya vizuri.
Amesema kumzuia mpinzani huyo bila kupata bao katika mechi hiyo kwake ni matokeo mazuri akibainisha kuwa Ligi haijaisha na ishu ya nafasi siyo tatizo kwani bado mashindano hayajaisha.
“Ushindi ni mchakato, suala la nafasi tulipo siyo tatizo, labda Ligi ingekuwa imefikia mwisho, kumzuia JKT Tanzania kwa sasa waliopo nafasi tatu za juu ni matokeo mazuri kwangu, naenda kurekebisha makosa tufanye vizuri,” amesema Otieno.
Kocha huyo ameongeza kuwa wapo wachezaji ambao hawakuwa na timu tangu mwanzo, lakini wameonesha ubora na kutengeneza nafasi ambazo hawakuwa na bahati kuzitumia.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally amesema hesabu na mipango yao ilikuwa ni kupata pointi tatu, lakini hata pointi moja ya ugenini si mbaya sana, huku akiwapongeza vijana wake kwa kazi nzuri.
Amesema katika mechi tano za nyuma waliweza kupata bao, lakini leo yapo makosa yameonekana hivyo kwa nafasi yake anaenda kuwajibika kurekebisha ili mechi zijazo waweze kuendeleza ubabe Ligi Kuu.
“Bado Ligi ni ngumu inahitaji kupambana kila mechi, tulijipanga kushinda ila hata pointi moja hii ni bora kwa kuwa Prisons walikuwa nyumbani na wameonesha upinzani,” amesema Ally.