:::::::::
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema imechangia kwa kiasi kikubwa katika kuhakikisha usalama wa nchi na wananchi wake, hususan katika maeneo ya mipakani, kupitia ukaguzi wa kina wa bidhaa zote zinazoingia nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo Januari 25, 2026 mkoani Dar es Salaam na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusufu Mwenda, wakati wa Bonanza la kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Forodha Duniani, ambapo alisema usalama uliopo nchini kwa sasa unatokana kwa kiwango kikubwa na utendaji kazi madhubuti wa TRA.
Mwenda alisema TRA imekuwa mstari wa mbele katika kudhibiti uingizwaji wa bidhaa hatarishi na zisizoruhusiwa, ikiwemo bidhaa bandia, dawa haramu na vitu vingine ambavyo havikidhi viwango vya kisheria, hatua inayolenga kulinda afya na usalama wa jamii.
Alibainisha kuwa pamoja na jukumu lake la msingi la kukusanya mapato kwa ajili ya maendeleo ya taifa, TRA imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kulinda jamii dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na bidhaa haramu.
“Hatuishii tu kukusanya mapato, bali pia tunahakikisha tunailinda jamii. Usalama wa wananchi ni kipaumbele chetu, na tutahakikisha tunawalinda kwanza watumishi wetu ili waweze kuilinda jamii kwa ufanisi zaidi,” alisema Mwenda.
Aidha, aliwataka wananchi kushirikiana na TRA kwa kutoa taarifa za vitendo vya kihalifu vinavyohusisha ukwepaji wa kodi na uingizwaji wa bidhaa haramu, akisisitiza kuwa ushirikiano huo ni nguzo muhimu katika kulinda usalama na uchumi.







