Serikali yazindua mwongozo wa kuongeza ujuzi kwa sekta ya kilimo

Iringa. Serikali imeendelea kuchukua hatua za kimkakati kuboresha sekta ya kilimo kwa kulenga kujenga nguvu kazi yenye ujuzi na stadi za kisasa, hatua inayotazamwa kuwa msingi wa mageuzi ya kilimo na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Hatua hiyo imebainishwa wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa Uratibu wa Mafunzo ya Kuongeza Ujuzi kwa Wafanyakazi wa Sekta ya Kilimo, uliofanyika katika Ukumbi wa Royal Palm, Manispaa ya Iringa, ukihusisha wakulima kutoka mikoa ya Iringa, Singida, Mbeya na Dodoma.

Akizindua mwongozo huo jana Jumamosi Januari 24, 2026, Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi), Rahma Kisuo, amesema mageuzi ya kilimo hayawezi kufikiwa bila kuwa na rasilimali watu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la sasa na la baadaye.

Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inaelekeza kubadili muundo wa nguvu kazi, hususan katika sekta ya kilimo, ili Taifa lijinasue kutoka kilimo cha mazoea na kuelekea kilimo cha tija na biashara.
“Mkazo unawekwa katika kuongeza ujuzi wa wakulima ili kilimo kiwe shughuli ya kiuchumi inayotumia teknolojia, mbinu bora za uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao,” amesema Kisuo.

Kupitia mafunzo hayo, wakulima na wasindikaji wadogo wamejengewa uwezo katika matumizi sahihi ya pembejeo, kilimo cha kisasa, usindikaji pamoja na mbinu za kuongeza thamani ya mazao. Mafunzo hayo yamelenga kuongeza ushindani wao katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Baadhi ya wakulima walionufaika na mafunzo hayo wamesema yamebadili mtazamo wao kuhusu kilimo na kuwawezesha kuongeza mavuno na kipato.

“Sasa tunaona mashamba kama biashara. Tofauti ya mavuno na kipato ni kubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma, na sasa tutalima kwa kuzingatia tija na soko,” amesema Peter Mpalanzi, mkulima wa Iringa.

Serikali imesema mwongozo huo utasaidia kuziba pengo la ujuzi lililokuwepo katika sekta ya kilimo, ambalo limekuwa kikwazo kwa uzalishaji wenye tija. Waajiri na wadau wa sekta hiyo wametakiwa kuwekeza zaidi katika mafunzo ya kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi wao ili kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia na ushindani wa soko.

Kuelekea mwaka 2050, Serikali inalenga kuwa na nguvu kazi yenye ujuzi wa kati kwa kiwango kikubwa huku utegemezi wa ujuzi wa chini ukipungua. Hatua hiyo inaelezwa kuwa msingi wa kuifanya sekta ya kilimo kuwa injini ya maendeleo ya viwanda, ajira na usalama wa chakula.

Meneja Mkuu wa Chama cha Ushirika mkoani Iringa (IFCU), Tumaini Lupola, amesema chama hicho kimekuwa mstari wa mbele kusambaza pembejeo zikiwamo mbolea za ruzuku, mbegu bora na viuatilifu, sambamba na kuwajengea uwezo wakulima.

Amesema pia IFCU inawatafutia wakulima masoko yenye uhakika, kujenga miundombinu ya uhifadhi wa mazao na kuanzisha miradi ya kuongeza thamani ili kuongeza kipato chao.

“Kupitia ruzuku ya mbolea na mbegu pamoja na mafunzo tunayoendesha, wakulima wameanza kuona matokeo ya moja kwa moja kwenye mavuno na kipato chao.

Tunaomba mafunzo haya yaendelee na kuwafikia wengi zaidi,” amesema Lupola.
Wataalamu wa maendeleo wanasema uwekezaji katika ujuzi wa wakulima ni kichocheo muhimu cha mageuzi ya kweli ya kilimo.

“Uwekezaji katika ujuzi wa wakulima ndiyo njia ya haraka ya kubadili kilimo kutoka cha mazoea kwenda cha kisasa. Bila nguvu kazi yenye ujuzi, malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 hayawezi kufikiwa,” amesema Paschal Mbata, mtaalamu wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kwa kuendelea kuwekeza katika mafunzo na uratibu wake, Serikali inalenga kuifanya sekta ya kilimo kuwa mhimili imara wa uchumi wa kipato cha kati na chachu ya kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.