Tanga. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewakataza wananchi, hususan kina mama, kuhifadhi fedha kwenye matiti ikieleza tabia hiyo huharibu ubora wa fedha na kuilazimisha Serikali kugharamia kuchapisha mpya kabla ya muda wake wa matumizi kuisha.
Mbali na kuhifadhi kwenye matiti, kufunga fedha kwenye pembe za kanga au vitambaa hali hiyo inasababisha fedha kujikunja na kuchakaa.
Kauli hiyo imetolewa leo Januari, Januari 25, 2026 na Ofisa Mwandamizi Mkuu wa Kurugenzi ya Mifumo ya Malipo ya Taifa, Kidee Mshihiri, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya wiki ya huduma za fedha kitaifa, yatakayofikia tamati kesho.
Mshihiri amesema endapo tabia ya kuhifadhi fedha kwenye matiti itaendelea, nyingi zitaharibika mapema hali itakayoongeza mzigo kwa Serikali kugharamia uchapishaji badala ya kuelekeza rasilimali hizo kwenye sekta muhimu za maendeleo.
“Fedha ni mhimili wa uchumi ambapo bila fedha, nchi haiwezi kusonga mbele.”
Ametumia nafasi hiyo kuomba fedha zihifadhiwe kwa ustaarabu ikiwemo kwenye pochi kama wanaume na kutoa elimu kwa jamii, akisema changamoto hiyo inahitaji juhudi za pamoja na uelewa wa wananchi wote.
Maafisa wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakitoa elimu ya huduma za kifedha kwa wananchi wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayofanyika jijini Tanga.
“Ninawaomba Watanzania wote watunze fedha hizi kwa njia sahihi, na yeyote mwenye uelewa huu awasaidie wengine kwa kutoa elimu kwa sababu tatizo ni kubwa na linahitaji hatua za haraka kutoka kwa jamii,” ameongeza.
Pia, amewatahadharisha wananchi wanaoshiriki sherehe na tafrija mbalimbali kuacha tabia ya kutupa fedha chini au kuzibandika kwenye paji la uso wa mwenye sherehe, akisema vitendo hivyo huharibu fedha na kuongeza gharama kwa Serikali.
“Ni vyema kutumia vyombo maalum vya kuhifadhia fedha wakati wa sherehe. Wengi hufanya vitendo hivi kwa kutojua, lakini ukweli ni kwamba vinachakaza fedha na kuigharimu Serikali baadaye,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa Umma wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Graciana Mahega, amesema wananchi wengi waliotembelea banda la benki hiyo walionyesha hamu ya kupata elimu ya fedha, ikiwemo uwekezaji kwenye hati fungani za Serikali na taratibu za kuzingatia wanapokopa ili kuepuka taasisi zisizo rasmi.
Mmoja wa wananchi waliotembelea banda hilo, Godrichi Mgamu, amesema amepata uelewa mpana kuhusu uwekezaji wa hati fungani za Serikali, akieleza kuwa awali alikuwa na mtaji lakini alishindwa kuwekeza kutokana na kukosa elimu ya kutosha.
Naye Bahati Mohamedi amesema,
“fedha si mali ya mtu mmoja tu leo ni zako kesho ni za mwingine. Zinapochakaa ni hatari kwa Taifa zima.”