Dakika 90 za kipa mpya zenye namba za kutisha

SIKU zote namba huwa haziongopi. Licha ya kuruhusu bao moja mbele ya Esperance ya Tunisia katika mechi ya Kundi D ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini dakika 90 alizotumika kwa mara ya kwanza kwa kipa mpya wa Simba, Djibrilla Kassali zimembeba kutokana na kazi kubwa aliyoifanya jijini Tunis.

Katika mechi hiyo, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Hammadi Agrebi uliopo mji wa Radès, jijini Tunis, Simba ilipoteza mechi hiyo kwa bao 1-0 kikiwa ni kipigo cha tatu mfululizo cha michuano hiyo na kuifanya isalie mkiani mwa kundi bila ya pointi, huku Esperance ikienda kileleni ikiwa na pointi tano (kabla ya mechi ya jana.)

Kassali aliyesajiliwa na Simba kupitia dirisha dogo lililo wazi hadi Januari 30 kuchukua nafasi ya Moussa Camara anayejiuguza goti, alicheza kwa dakika zote 90 mechi hiyo ya tatu kwa Simba katika hatua ya makundi.

Kipa huyo raia wa Niger alikoa michomo mitatu ya hatari, huku akionekana mtulivu langoni licha ya changamoto ndogondogo zilizoonekana hasa za kimawasiliano na ukuta wake, huku akiwa na asilimia 0.08 ya kulinda lango kulinganisha na kipa wa Esperance, Ben Said aliyekuwa na 0.04.

KIP 01


Mbali na kuokoa michomo hiyo, Kassali alijaribu pia kuanzisha mashambulizi. Alionyesha ustadi wa kupiga pasi ambapo alitimiza 19 kati ya 24 za pasi sahihi, sawa na asilimia 79, pia akigusa mpira mara 30.

Hata hivyo, katika robo ya mwisho ya uwanja usahihi wake ulikuwa mdogo zaidi, akiwa na pasi moja sahihi kati ya tatu (33%). Pasi zake za mbali zilikuwa na ufanisi wa asimia 58% (7 kati ya 12).

Pia alivyokuwa ametulia langoni kulifanya baadhi ya mashabiki kupitia mitandao ya kijamii kumsifia kwamba angalau wameanza kuwa na amani langoni baada ya kukosekana kwa Camara na Yakoub Suleiman aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu huu kabla ya kuumia akiwa na timu ya taifa, Taifa Stars iliyoshiriki FCON 2025.

KIP 02


Rekodi zinaonyesha kuwa, Camara katika mechi ya kwanza kuichezea Simba katika michuano hiyo msimu uliopita ilikuwa Septemba 20, 2025 katika hatua za awali ambapo aliiongoza timu hiyo kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Gaborone United, aliokoa michomo miwili ya hatari.

Msimu uliopita aliisaidia timu hiyo, kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo ilipoteza kwa jumla ya mabao 3-1 dhidi ya RS Berkane ya Morocco baada ya kupigwa kwa fainali mbili, huku Camara akishika nafasi ya pili kwa clean sheet nyingi akiwa sita nyuma ya kipa wa RS Berkane, Mohammed Munir aliyekuwa na tisa.

KIP 03


Ni ngumu kumtupia lawama kwa bao ambalo aliruhusu katika mechi hiyo, yalikuwa ni makosa ya beki wa kulia, Shomary Kapombe ambaye alizidiwa ujanja na Mburkinabe, Jack Diarra kufuatia pasi ya Ben Hamida.

Hata hivyo, Kassali  bado ana dakika 90 nyingine wikiendi ijayo dhidi ya haohao, Esperance ambazo Simba inahitaji ubora wake ili kufufua matumaini ya kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika licha ya kuvurunda katika mechi tatu za kwanza na kuweka rekodi mbovu zaidi. 

Simba ilianza kwa kupoteza 1-0 mbele ya Petro Atletico ya Angola ikiwa nyumbani, kisha kulala ugenini kwa mabao 2-1 ilipoumana na Stade Malien ya Mali kabla ya kipigo hicho cha juzi kilichozidi kuiweka pabaya.

KIP 04


Kocha wa zamani wa makipa wa Simba na Azam FC, Daniel Cadena anaamini kipa huyo Mnaija atakuwa msaada kwa wekundu wa Msimbazi hao katika kipindi hiki kigumu; “Hiki ni kipindi ambacho klabu yoyote inaweza kupitia kikubwa ni kuendelea kuamini katika mpango na kila kitu kitakaa sawa,”

Aliongea kwa kusema; “Anaonekana ni kipa mzuri na mwenye uzoefu wa kutosha, lakini mara zote nimekuwa nikisema jukumu la lango kuwa salama sio la kipa tu, timu yote inatakiwa kuwa sawa. Ikiwa na maana kila idara hususani mabeki. Akiendelea kuaminiwa ataibeba kama ilivyokuwa kwa Camara na wengine.”