MSANII mkongwe wa filamu za Kibongo, Omary Babuu ‘Bambucha’ amesema japo yeye ni shabiki wa Simba, lakini anatamani kile kinachofanywa na Yanga kinastahili kuigwa na timu hiyo anayoishabiki ili iweze kurejea katika ushindani na kuleta furaha kwa mashabiki wa klabu hiyo ya Msimbazi.
Bambucha aliyewahi kutamba na filamu ya Sura Mbili, amesema Yanga kwa misimu ya karibu imekuwa na wachezaji wenye uwezo wa hali ya juu na kujituma uwanjani akiwamo Pacome Zouzoua ambaye msimu uliopita alimaliza na mabao 12 na asisti 10. Pia aliwataka Prince Dube aliyemaliza na mabao 13 asisti nane, huku Maxi Nzengeli akifunga sita na kusisti 10 pamoja na kipa Djigui Diarra alikuwa na clean sheets 17.
“ Simba irejee katika kauli yake ya Nguvu Moja kwa sasa kinachoendelea ni nguvu 100, kikosi cha Yanga kina wachezaji wenye uwezo mkubwa, kilichonishangaza usajili unaoendelea uongozi wa Simba unakwenda kuzungumza na Allan Okello halafu injinia Hersi Said anakwenda kumsajili, hilo linaonyesha ubabaifu,” amesema Bambucha na kuongeza;
“Simba kuna wachezaji wazuri kama Elie Mpanzu, lakini anakimbia kwa kasi kuna wakati anaacha mpira nyuma, humuoni katika mechi ngumu anafanya maamuzi kama ilivyo kwa Pacome, kuna Kibu Denis anatumia nguvu kubwa akifika langoni hakuna anachokifanya, ili awe mfungaji mzuri basi arekebishe hilo”.
Mwigizaji huyo amesema isingekuwa majeraha kumweka nje ya kazi kipa Moussa Camara aliyemaliza na clean sheets 19 msimu uliyopita angeisaidia Simba katika michuano mbalimbali kwa msimu huu.
“Simba wakae chini waangalie wanapokosea wasiendelee kushusha brandi ya timu kwa kuwapa kichwa Yanga, wale ni watani wa jadi, endapo kama hawatakubali kurekebisha changamoto basi mashabiki tutaendelea na maumivu,” amesema Bambucha.
Simba inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika imetoka kupoteza mechi ya tatu mfululizo ya Kundi D baada ya kulala 1-0 ugenini mbele ya Esperance ya Tunisia, huku ikiwa haijashinda mechi yoyote ya nyumbani ya michuano hiyo msimu huu ikicheza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa itakaorudiana na Watunisia hao.