WPL kuendelea Jumatano kwa mechi tano

MTANANGE wa Ligi Kuu ya Wanawake itaendelea tena Jumatano hii Januari 28 zikipigwa mechi tano ikiwemo ile ya bingwa mtetezi JKT Queens dhidi ya Alliance Girls inayotarajiwa kuwa na ushindani.

Msimamo wa ligi hadi sasa unaongozwa na Simba yenye pointi 28 ikifuatiwa na Yanga Princess yenye nazo 24, JKT nafasi ya tatu na pointi 20 huku Alliance ikiwa nafasi ya nne na pointi 19.

Mechi zote za raundi ya 11 zitapigwa saa 10 jioni pale Uwanja wa KMC, Tausi FC ataikaribisha Ceasiaa Queens, Ruangwa Queens v Fountain Gate (Majaliwa), Bunda Queens v Yanga Princess (Karume), Mashujaa v Bilo Queens (TFF Kigamboni) na JKT V Alliance (Mej Gen Isamuhyo).

Akizungumzia mechi hiyo Kocha wa Ceasiaa, Ezekiel Chobanka amesema hawakuwa na matokeo mazuri mwanzoni lakini wameweka mpango mkakati wa kupata pointi tatu kwa kila mechi.

“Hatukuwa na matokeo mazuri na hatuko sehemu nzuri kwenye msimamo tunakwenda kucheza na Tausi wakiwa kwao nyumbani hatutadharau mechi hiyo na tunakwenda kupigania pointi tatu muhimu ingawa haitakuwa rahisi.”

Kocha wa JKT, Abdallah Kessy amesema wanafahamu ubora wa Alliance msimu huu na dhamira yao ni kushinda kila mechi ili kuhakikisha wanatetea taji la ligi.

“Tumewafuatilia wapinzani wetu wanacheza vizuri ligi msimu huu imekuwa ngumu kila timu inapambania pointi tatu hivyo kwetu tumejipanga kuhakikisha tunachukua pointi.”