Ndoto za RPC wa zamani kupinga ubunge wa Kakulu wa CCM zayeyuka

Dar es Salaam. Kada wa Chama cha ACT Wazalendo, Jamal Rwambow, amejikuta njia panda kupinga ushindi wa mbunge wa Mbagala (CCM), Kakulu Burchard, baada ya kesi aliyoomba aunganishwe nayo kuondolewa mahakamani.

Katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, Rwambow aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi (RPC) katika mikoa mitatu nchini kabla ya kustaafu, alikuwa mwanachama wa CCM kabla ya kujiunga na ACT Wazalendo Agosti 5, 2025.

Baada ya kujiunga na ACT Wazalendo, chama hicho kilimdhamini kugombea ubunge wa Mbagala jijini Dar es Salaam, sambamba na wagombea wengine akiwamo Kakulu na mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Said Kinyogoli.

Rwambow hakuridhika na matokeo yaliyompa ushindi Kakulu akajaribu kufungua shauri la uchaguzi Mahakama Kuu masjala ndogo ya Dar es Salaam, lakini akakumbana na kikwazo baada ya kuwasilisha shauri nje ya siku 30 za kisheria.

Lakini Kinyogoli alifanikiwa kufungua shauri la uchaguzi namba 28283 la 2025 dhidi ya Kakulu kama mlalamikiwa wa kwanza, msimamizi wa uchaguzi Mbagala na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kama mlalamikiwa wa pili na wa tatu.

Rwambow hakukata tamaa, akafungua maombi namba 000032773 ya mwaka 2025 dhidi ya Kinyogoli, Kakulu, Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Mbagala na AG, akiomba mahakama imuunganishe katika shauri hilo lililofunguliwa na Kinyogoli.

Kupitia maombi hayo, Rwambow aliiomba Mahakama, aunganishwe kama mlalamikiwa wa nne, gharama za shauri zilipwe na mjibu maombi wa pili, wa tatu na wa nne na nafuu nyingine ambayo Mahakama itaona inafaa kuzitoa.

Hata hivyo, wakati maombi yake hayo yalikuwa yamepangwa kutajwa Februari 23, 2026 mbele ya Jaji Hussein Mtembwa wa Mahakama Kuu, masjala ndogo ya Dar es Salaam, Kinyogoli ameamua kuondoa shauri la uchaguzi alilolifungua.

Hii maana yake maombi ya Rwambow yanakuwa yamekufa kifo cha asili kwa kuwa kisheria hayawezi kusimama bila kuwapo kwa shauri la msingi la Kinyogoli, ambalo mgombea huyo alikuwa anaomba kuunganishwa ili kupinga ushindi wa Kakulu.

Kinyogoli alipotafutwa kwa simu jana, alisema anaingia msikitini kuswali hivyo atafutwe baada ya dakika 15 lakini muda huo alipopigiwa hakupokea simu na hata alipopigiwa simu baadaye pia iliita bila majibu.

Hata hivyo wakili wake, Mashaka Ngole kutoka kampuni ya uwakili ya Ngole & Associates Law Chamber ya Jijini Dar es Salaam alithibitisha Kinyogoli kuondoa shauri hilo la uchaguzi kwa ridhaa yake, japo hakueleza aliliondoa lini.

“Mleta shauri ameamua kuondoa shauri la uchaguzi alilokuwa amefungua kwa hiyo hata yale maombi (ya Rwambow) yatakufa kwa sababu hakuna kesi ya msingi ambayo maombi yake ndio yaliegemea,” alisema wakili Ngole.

Rwambow mwenyewe alipotafutwa na Mwananchi jana Jumapili Januari 25,2026 alisema anasubiri kufahamu mahakama itasema nini hiyo Februari 23, 2026 siku ambayo maombi yake yamepangwa kutajwa, lakini akasema kuna kitu amejifunza.

“Hii imeniongezea mambo ya kuandika kwenye kitabu changu. Huu uchaguzi umenifundisha mambo mengi. Kama shauri la msingi nililolitegemea halipo automatically (moja kwa moja) maombi yangu yatakufa,” alisema Rwambow.

Katika shauri hilo la uchaguzi, Kinyogoli alikuwa ameiomba Mahakama amri nne, moja, Mahakama Kuu itoe tamko kwamba uchaguzi wa ubunge Jimbo la Mbagala uliofanyika Oktoba 29 ni batili na ulitawaliwa na ukiukwaji wa sheria za uchaguzi.

Pili, Mahakama Kuu itoe tamko kwamba Kakulu hakuchaguliwa kihalali kuwa mbunge wa jimbo hilo, tatu, Mahakama itoe amri ya kurudiwa kwa uchaguzi wa Jimbo la Mbagala na nne, Kakulu aamriwe kulipa gharama za shauri hilo.

Kuondolewa kwa shauri hilo kunazima ndoto ya Rwambow kupinga matokeo hayo kwa kupitia shauri hilo la Kinyogoli ambalo ameamua kuliondoa kortini na sasa Kakulu ni miongoni mwa wabunge ambao ushindi wake haupingwi kortini.