::::::::::;
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kuwa utabiri wa mvua za Vuli unaoendelea kwa sasa umefanikiwa kwa kiwango cha usahihi wa asilimia 94.1, hali inayoonesha uwezo mkubwa wa kitaalamu katika sekta ya utabiri wa hali ya hewa nchini.
Akizungumza na Torch Media katika mahojiano maalumu yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mtaalamu wa Hali ya Hewa kutoka TMA, Alfred Kondoya, amesema hali ya mvua na mwenendo wa hali ya hewa uliojionesha umeendana kwa kiwango kikubwa na makadirio ya awali ya kitaalamu.
Amesema kiwango cha mvua kilichonyesha pamoja na mwelekeo wake katika maeneo mbalimbali nchini kimekuwa kikilingana na asilimia za utabiri uliotolewa na mamlaka hiyo, jambo linaloonesha usahihi wa takwimu zilizotumika.
Hata hivyo, Kondoya amesema mvua za Vuli zimekuwa na mtawanyiko usio wa kawaida katika baadhi ya maeneo, hali iliyosababisha athari kwa shughuli za kilimo, hasa kwa wakulima waliotegemea ratiba maalumu ya msimu wa upandaji.
Kutokana na hali hiyo, TMA imewataka wananchi pamoja na wadau mbalimbali kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa mara kwa mara ili kuchukua tahadhari stahiki mapema.
Wakati huo huo, TMA imesema inatarajia kutoa rasmi utabiri wa mvua za Masika mwanzoni mwa mwezi Februari mwaka huu, utabiri ambao utahusu kipindi cha kuanzia mwezi Machi hadi Mei.
Kondoya amesema utabiri huo ni muhimu kwa mipango ya sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, maji, nishati na miundombinu, hivyo amewataka wananchi kuwa wavumilivu kusubiri tangazo rasmi ili kupata mwelekeo sahihi wa msimu wa Masika.
Ameongeza kuwa kabla ya kutangaza utabiri huo, TMA imekuwa ikifanya vikao vya mashauriano na taasisi za Serikali na wadau mbalimbali ikiwemo DAWASA, Wizara ya Maji, Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na taasisi nyingine, kwa lengo la kubaini changamoto na kutoa ushauri wa kitaalamu kulingana na mahitaji ya maeneo husika.
