WATENDAJI WA UCHAGUZI WATAKIWA KUTEKELEZA MAJUKUMU KWA WELEDI

Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya

Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk akizungumza leo

tarehe 26 Januari, 2026 mkoani Iringa wakati akifunga mafunzo ya siku tatu ya watendaji

wa uchaguzi kutoka Halmashauri za Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma na

Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe.(Picha na INEC).

Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya

Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk akizungumza leo

tarehe 26 Januari, 2026 mkoani Iringa wakati akifunga mafunzo ya siku tatu ya watendaji

wa uchaguzi kutoka Halmashauri za Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma na

Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe.

Meza Kuu ikiongozwa na Mwenyekiti wa Tume, Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele ikiwa katika ufungaji wa mafunzo hayo.

Na. Mwandishi Wetu, Iringa

Watendaji wa uchaguzi wametakiwa kutekeleza

majukumu yao kwa ufanisi na weledi ili kufanikisha uchaguzi mdogo wa ubunge

katika Jimbo la Peramiho na udiwani katika Kata ya Shiwinga unaotarajiwa

kufanyika tarehe 26 Februari, 2026.

 

Wito huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa (Mst) Mbarouk

Salim Mbarouk Mkoani Iringa leo tarehe 26 Januari, 2026 wakati akifunga mafunzo

ya watendaji wa uchaguzi yaliyofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 24 Januari,

2026.

 

“Ni matazamio ya Tume kwamba, baada ya

kupatiwa mafunzo haya, mtatekeleza majukumu yenu kwa ufanisi na weledi

mkizingatia ratiba ya utekelezaji ili kufanikisha uchaguzi mdogo wa ubunge

katika Jimbo la Peramiho na Udiwani katika Kata ya Shiwinga unaotarajiwa

kufanyika tarehe 26 Februari, 2026,” amesema Jaji Mbarouk.

 

Amesisitiza kuwa ili ufanisi uwepo ni muhimu

watendaji hao wazingatie sifa na uwezo wakati wa kuteua na kuajiri watendaji wa

vituo vya kupigia kura kwa kuwa hao ndio watakaosimamia zoezi la kupiga kura na

kuhesabu kura vituoni.

 

“Kuhusu ajira za kupata watendaji wa vituo,

tunayo imani kuwa mtateua na kuajiri watendaji wenye sifa na uwezo wa kufanya

kazi hii muhimu……kwa kuwa hao ndio watakaosimamia zoezi la kupiga kura na

kuhesabu kura vituoni. Kazi ambayo inahitaji umahiri, umakini na weledi katika

kuitekeleza,” amesema Jaji Mbarouk.

 

Amewataka watendaji hao kuhakikisha kuwa

mafunzo ya watendaji wa vituo yanafanyika kwa ufanisi na weledi katika tarehe

zilizopangwa kwenye ratiba ya utekelezaji wa shughuli za uchaguzi.

 

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga

kuwajengea uwezo ili waweze kufahamu majukumu yao na kuyatekeleza ipasavyo

wakati wa uchaguzi.

 

Jaji Mbarouk amewakumbusha watendaji hao kuwa

shughuli zote za uchaguzi zinaongozwa na Katiba, sheria, kanuni, maadili ya

uchaguzi na maelekezo ya Tume na kuongeza kuwa kuna umuhimu wa kutenga sehemu

ya muda wao kusoma Katiba, sheria na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume

ili yawaongoze katika kusimamia uchaguzi utakaokuwa huru na wa haki.

 

Mafunzo hayo yamewahusisha Waratibu wa

Uchaguzi wa Mikoa ya Songwe na Ruvuma, Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi

Wasaidizi wa Uchaguzi Ngazi ya Jimbo, Wasimamizi wa Uchaguzi Ngazi ya Kata,

Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ununuzi na Wahasibu.

 

Mada kadhaa ziliwasilishwa ikiwa ni pamoja na

Majukumu ya Watendaji wa Uchaguzi, Mambo Muhimu ya Kuzingatia, Uteuzi wa

Wagombea, Maadili na Kampeni za Uchaguzi, Wajibu na Majukumu ya Watendaji wa

Vituo na Utambulisho wa Mawakala wa Vyama vya Siasa, Taratibu za Upigaji Kura,

Taratibu za Kuhesabu Kura, Kujumlisha Kura na Kutangaza Matokeo, Fomu

Zinatotumika kwenye Uchaguzi, Mapokezi na Utunzaji wa Vifaa vya Uchaguzi na

Usimamizi wa Fedha za Uchaguzi.