BoT Yawakumbusha Wananchi Kutunza Fedha Ili Kuepuka Kuharibika kwa Noti



Wananchi wamekumbushwa umuhimu wa kutunza fedha kwa kuziweka katika mazingira salama ili kuepusha kuharibika kwa ubora wa noti na changamoto za kiafya.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayofanyika kitaifa jijini Tanga, Afisa Mwandamizi Mkuu kutoka Kurugenzi ya Mifumo ya Malipo ya Taifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kidee Mshihiri, amesema bado baadhi ya wananchi wana tabia zisizo sahihi za kuhifadhi fedha.

Ameeleza kuwa tabia ya kuweka fedha kwenye matiti husababisha noti kulowa jasho, kuchafuka na kupoteza ubora wake mapema, hali inayozifanya zisitumike kwa muda mrefu. Aidha, amesisitiza kuwa tabia hiyo pia ni hatari kwa afya.

“Mfano mwingine wa tabia zisizofaa ni kushika fedha, hususani noti, ukiwa na vumbi la mkaa au kuzifunga kwenye khanga au kitenge, kwani hali hiyo husababisha fedha kuchafuliwa na kuharibiwa,” amesema Mshihiri.

BoT imetoa wito kwa wananchi kuhifadhi fedha katika pochi, mkoba au sehemu safi na salama ili kulinda ubora wa noti na kuhakikisha zinaendelea kutumika kwa muda mrefu.

Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya fedha na huduma za kifedha nchini.