Ofisa wa Polisi afichua mipango ya kumshambulia Gachagua kanisani

Ofisa mmoja wa Polisi ameliambia Daily Nation la Kenya kuwa kikosi cha maofisa 15 kilikusanywa Nairobi Ijumaa na kupewa kibali jioni hiyo kwenda kuvuruga ibada katika Kanisa la Witima ACK.

Mashambulizi ya kikatili yaliyofanyika Jumapili dhidi ya aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, wakati wa ibada ya kanisani Othaya, Kaunti ya Nyeri, yanadaiwa kupangwa siku kadhaa kabla jijini Nairobi huku maagizo yakitolewa kuhakikisha polisi wa eneo hawahusishwi.

Ofisa huyo alieleza kuwa kikosi hicho kilielekezwa kushirikiana na vijana wapatao 20 kutoka Kaunti ya Nyeri, huku polisi wa eneo husika waliamriwa kutojihusisha.

“Tulipewa kibali Ijumaa jioni kwenda kuvuruga ibada ya Gachagua. Polisi wa eneo waliamriwa mapema wasijihusishe,” alisema.

Kikao cha kupanga shambulizi hilo kiliitishwa na maofisa wawili waandamizi walioko Vigilance House, Nairobi, pamoja na viongozi watatu kutoka Mlima Kenya, akiwamo mmoja mwanamke.

Mashuhuda walisema wakazi walikimbia kuokoa maisha yao baada ya makopo ya gesi ya machozi kurushwa ndani ya kanisa, huku wanaume wasiopungua 15 waliokuwa na silaha, wanaodhaniwa kuwa maofisa wa polisi, wakiingia eneo hilo na kuanza kufyatua risasi.

Shambulio hilo lilidumu zaidi ya dakika 30, likiacha magari yakiwemo ya Gachagua yamevunjwa vioo, milango ya kanisa ikiwa na mashimo ya risasi, na baadhi ya madirisha yalivunjika.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kipchumba Murkomen, alilaani shambulizi hilo na kumwagiza Mkuu wa Polisi, Douglas Kanja, kuwafuatilia mara moja waliohusika.

Alisisitiza kuwa vurugu popote, hasa mahali pa ibada, hazikubaliki na wahusika watafikishwa mbele ya sheria.

Gachagua alihoji kwamba shambulio hilo lilikuwa jaribio la kumuua, akilaumu serikali kwa kuliruhusu. Alidai washambuliaji walitoka kwenye kikosi hatari cha polisi kinachohusishwa na utekaji nyara na mauaji ya kiholela, wakiwemo wabunge wawili kutoka Nyeri na Murang’a.

Alionya kuwa kuna kiwango cha vitisho anachoweza kuvumilia na alishutumu serikali kwa kuandaa mazingira ya ukandamizaji kuelekea uchaguzi wa 2027.

Naibu Rais wa Kenya, Kithure Kindiki, alilaani tukio hilo, akisema vurugu mahali pa ibada hazikubaliki, bila kujali mpangaji.

Alisisitiza kuwa uchunguzi huru, usioegemea siasa, ni njia pekee ya kuhakikisha vurugu hazichukui nafasi ya ushindani wa kidemokrasia.

Mbunge wa Laikipia Mashariki, Mwangi Kiunjuri, alihoji madai ya Gachagua na kumtaka aendelee kurekodi taarifa rasmi kwa polisi, akishutumu baadhi ya vyombo vya usalama kwa kushirikiana na Gachagua na kuitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina.

Msemaji wa Huduma ya Polisi ya Taifa (NPS), Muchiri Nyaga alisema Mkuu wa Polisi ameagiza Kitengo cha Masuala ya Ndani (IAU) kuanza uchunguzi mara moja, huku Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Kati akielekeza Ofisa wa Upelelezi wa Jinai wa Kaunti (CCIO) Nyeri kuhifadhi eneo la tukio na kuanza uchunguzi.

Nyaga alisisitiza kuwa NPS inapinga vurugu za aina yoyote na watakaobainika kuhusika watachukuliwa hatua kali na za haraka.

Aliongeza kuwa makanisa ni maeneo matakatifu na hayapaswi kuhusishwa na vurugu au siasa.