Dar es Salaam. Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote umeanza rasmi leo, Januari 26, 2026, ukiwa na lengo la kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya bila kikwazo cha fedha.
Mpango wa utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (Universal Health Insurance Act, 2023) umeanza rasmi jana baada ya Wakuu wa Mikoa kote nchini kuanza kusimamia usajili wa kundi la kaya maskini. Kundi hili lenye jumla ya kaya 276,000 limechaguliwa kuwa la majaribio ya mfumo wa bima ya afya kwa wote, kabla ya makundi mengine kuanza kujiunga.
Akizungumza na Mwananchi, Meneja Uhusiano kwa Umma wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), James Mlowe, amesema kundi hilo litaanza kwa majaribio ili kuona kama mifumo inafanya kazi vizuri.
Aidha, jaribio hilo litawawezesha kubaini namna ya kugawanya rasilimali ikiwemo watendaji, dawa na vifaatiba, ili makundi mengine yakianza kusajiliwa wawe tayari.
“Kuanzia leo usajili umeanza kwa kaya 276,000 na tunatarajia mchakato huu utaendelea mwezi mmoja hadi mwezi na nusu. Orodha itaonyesha wanatoka vijiji gani, kuwafuata, kuwasajili na kuwatolea vitambulisho, jambo linalohitaji muda kidogo.”
“Baada ya kukamilika, kaya hizi zitaunganishwa na vituo vya afya vitakavyowahudumia na kuanza kupata huduma,”amesema Dk Mlowe.
Mganga Mkuu Mkoa wa Mbeya, Dk Elizabeth Nyema amesema Serikali mkoani humo tayari wamejipanga baada ya kutoa elimu ya awali tangu Desemba 2025, na sasa wapo katika hatua za mwisho kuanza usajili rasmi.
Aidha, Wakurugenzi wa Halmashauri za Mbarali, Mbeya na Kyela wameshaanza kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa bima ya afya kwa wote, wakihakikisha wananchi wanajua, wanajiandaa na kupata huduma hiyo.