Chikola afunguka kutua Singida Black Stars

UONGOZI wa Yanga umemtoa kwa mkopo kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Offen Chikola kwenda Singida Black Stars, huku mwenyewe akisema hiyo kwake ni sehemu ya kumjenga zaidi.

Chikola aliyejiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu huu akitokea Tabora United ambayo kwa sasa inafahamika kwa jina la TRA United, ametolewa kwa mkopo wa miezi sita ili apate muda mwingi wa kucheza baada ya kuonekana nafasi yake ni finyu mbele ya Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga kimeliambia Mwanaspoti kuwa: “Sio mchezaji mbaya, ana uwezo mkubwa na ndio maana alipata nafasi ya kusajiliwa ndani ya Yanga. Kilichomuondoa ni kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara kama kule alipokuwepo.

“Yeye kama mchezaji anatamani kuona anapata walau dakika nyingi za kucheza, baada ya kupata dakika chache aliomba atolewe kwa mkopo na ndicho kilichofanyika.”€

Mwanaspoti limepata nafasi ya kumtafuta Chikola ambaye amesema, “taarifa za mimi kutolewa kwa mkopo ni za kweli, naenda Singida Black Stars, ni muda sahihi wa mimi kwenda kutafuta changamoto nyingine ya kupambania namba kikosi cha kwanza, kazi yangu ni mpira, hivyo nataka kuitumikia kwa kucheza.

“Naheshimu namba kubwa ya wachezaji waliopo kwenye timu, hivyo juhudi na kuamini katika kuwekeza nguvu ya kufanya mazoezi kwa nguvu vitanipa nafasi ya kucheza. Yanga imekuwa darasa kubwa kwangu.”