Kibaha. Walimu wa shule za msingi na sekondari katika Manispaa ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, wametakiwa kuwatambua wanafunzi kulingana na mazingira wanakotoka ili waweze kutumia mbinu sahihi za ufundishaji zitakazowawezesha kuelewa masomo na kuongeza kiwango cha ufaulu.
Wito huo umetolewa leo Jumatatu Januari 26, 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa madawati 4,000 kwa shule za msingi na sekondari zilizopo katika manispaa hiyo.
Simon amesema baadhi ya wanafunzi wanatoka katika mazingira magumu yakiwamo ya familia zisizo na utulivu, watoto yatima, wanaoishi na mzazi mmoja au wanaokosa malezi yenye upendo, hali ambayo inaweza kuathiri mwenendo wao wa kitaaluma endapo haitatambuliwa mapema.
Amesisitiza kuwa walimu wakiwafahamu wanafunzi wao pamoja na changamoto zinazowakabili, watakuwa na nafasi kubwa ya kutumia mbinu stahiki za ufundishaji zitakazowawezesha kuelewa masomo na kufanya vizuri shuleni.
Agizo hilo linatolewa wakati Manispaa ya Kibaha ikiendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuboresha elimu, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya shule, upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na ufuatiliaji wa ufundishaji kupitia idara ya elimu.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani Nickson Simon akikata utepe kuashiria uzinduzi wa ugawaji wa madawati kwa Shule za Msingi na Sekondari Manispaa ya Kibaha leo Januari 26, 2026. Picha na Sanjito Msafiri
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dk Rogers Shemwelekwa amesema madawati hayo yanayojumuisha meza na viti, yamegharimu jumla ya Sh400 milioni, fedha zilizotokana na mapato ya ndani ya manispaa hiyo.
Amesema uwekezaji huo unalenga kuboresha mazingira ya ujifunzaji, kuongeza ari ya wanafunzi kuhudhuria masomo na hatimaye kuinua kiwango cha ufaulu.
Mmoja wa walimu kutoka shule zilizopokea madawati hayo, Primitiva William amesema maelekezo yaliyotolewa yana uzito mkubwa na walimu wapo tayari kuyatekeleza ili kuhakikisha kila mwanafunzi anapata haki yake ya msingi ya elimu.
Naye Omary Khatibu, mzazi katika Manispaa ya Kibaha, amesema kuboreshwa kwa mazingira ya kujifunzia kutachochea tija katika sekta ya elimu kwa kuwa wanafunzi hupenda kusoma katika mazingira rafiki na salama.
Kwa upande wake, mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mkoani, Peter Msafiri amesema upatikanaji wa madawati hayo umeondoa changamoto ya wanafunzi kusoma wakiwa wamekaa chini, hali iliyoongeza hamasa na ari ya kujifunza.
