KIFO cha kipa wa zamani wa Taifa Stars, Yanga, Sigara na Mtibwa Sugar, Peter Manyika Sr kimewaliza wachezaji mbalimbali hapa nchini, huku wakimzungumzia kwa nyanja tofauti namna walivyofanya naye kazi wakati wa uhai wake.
Mbali na kuwa mchezaji enzi za uhai wake, Manyika amewahi kuwa kocha wa makipa wa Yanga, Ihefu ambayo sasa inaitwa Singida Black Stars, Singida Fountain Gate, Namungo na timu mbalimbali za Taifa.
Mwanaspoti lilipata taarifa ya kifo chake, kutoka kwa kijana wake Manyika Peter Jr ambaye ni kipa wa zamani wa Simba na baba yake alifariki alfajiri ya Januari 26, 2026 katika Hospitali ya St. Monica jijini Dar es Salaam wakati akipatiwa matibabu.
“Baba alifariki akiwa anatibiwa hospitali ya St. Monica, lakini kwa sasa nahitaji utulivu kwanza siwezi kuzungumza mambo mengi,” amesema Manyika aliyewahi kucheza Ligi Kuu Kenya katika klabu ya KCB.
Kipa wa TRA United, Fikirini Bakari alizungumzia namna alivyofanya naye kazi akiwa Ihefu akisema: “Alikuwa zaidi ya kocha, ni baba wa wachezaji wengi, ambacho sitakisahau alinipa moyo nipambane nitakuwa mkubwa, hakuna aliyezaliwa mkubwa.”
Kwa upande wa nahodha wa Namungo, Jacob Masawe, amesema: “Nakumbuka mechi dhidi ya Tanzania Prisons, licha ya kushinda 1-0 ugenini lakini nilikosa bao la wazi alifoka sana, baada ya mechi alinifuata na kuniambia nia yangu haikuwa mbaya, nilitaka uongeze umakini zaidi, alikuwa mshauri, alisimama kama baba.”
Staa wa zamani wa Simba, Meddie Kagere amesema: “Tanzania imepoteza mtu muhimu lakini ni kazi ya Mungu, alikuwa kocha mshauri anayependa watu wafanikiwe.”
Kagere aliyewahi pia kuichezea Singida Black Stars na Namungo aliongeza: “Inaumiza lakini nawapa pole familia na watu wake ambao wameguswa na msiba huo.”
Mwenyekiti wa Chama cha Wachezaji Zamani wa Mpira wa Miguu Tanzania (Galacticos), Ally Mayay Tembele, amesema ni msiba mzito na kazi aliyoifanya akiwa kipa wa Yanga na Taifa Stars, itaendelea kukumbukwa daima.
Mayay amesema alicheza na Manyika Sr wakiwa Yanga, pia walikuwa wanakutana mara kwa mara, hivi karibuni walikwenda kumuona hospitali ya Taifa ya Muhimbili na walikuwa wanapiga naye stori.
Kwa upande wa Idd Moshi, staa wa zamani wa Yanga na mtunza hazina wa Galacticos, amesema: “Kifo ni fumbo kwani hakuwa na dalili za kumuona kazidiwa, alikuwa kawaida na tulikuwa tunapiga naye stori za soka.”