Ouma aiona robo fainali Shirikisho

BAADA ya kuambulia pointi tatu nyumbani dhidi ya AS Otoho, Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma amesema anaiona nafasi ya timu hiyo kuendelea kuandika historia kwa kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Ushindi wa Singida Black Stars juzi Jumapili wa bao 1-0 dhidi ya AS Otoho kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, umeifanya timu hiyo kufikisha pointi nne ikishuka dimbani mara tatu na kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi C sawa na Stellenbosch, huku CR Belouizdad ikiongoza na pointi sita. AS Otoho inazo tatu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma amesema haikuwa rahisi kwao lakini wamefanya kile walichokuwa wanastahili kufanya huku akitaja siri ya mafanikio ya kuibuka na pointi tatu nyumbani ni wachezaji kufuata maelekezo.

“Ulikuwa ni mchezaji muhimu kwetu kupata matokeo haya, wachezaji walicheza kwa nidhamu na kumuheshimu mpinzani, baada ya matokeo haya naiona nafasi yetu ya kutinga hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza huku tukiendelea kuandika historia.

“Malengo yalikuwa kutinga hatua ya makundi kwa mara ya kwanza, tumefanikiwa na sasa matamanio ni kusonga mbele zaidi, hili linawezekana kama tutaendeleza nidhamu ya uchezaji na kufanyia kazi kila tunachoelekezana,” amesema Ouma.

Ouma aliwapongeza wachezaji kupambania timu hiyo huku akiamini walichokifanya katika michuano hiyo watakihamishia Ligi Kuu Bara ili kutafuta nafasi nyingine ya uwakilishi msimu ujao.

“Singida Black Stars ni timu kubwa kuna wachezaji wakubwa na bora. Tuna kila sababu ya kuzoea kushiriki michuano ya kimataifa ili kujijengea uimara na uzoefu kupambania nafasi.”