Geita. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeingilia kati mgogoro wa matumizi ya ardhi unaohusisha Halmashauri ya Wilaya ya Geita na mwekezaji katika eneo la Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro, mkoani Geita, kufuatia mvutano uliosambaa kupitia mitandao ya kijamii.
Hatua hiyo imechukuliwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ikiwa ni juhudi za Serikali kuhakikisha mgogoro huo unashughulikiwa kwa kina na kufikia muafaka wa kisheria.
Kwa mujibu wa tamko lililotolewa leo Januari 26, 2026 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Leonard Akwilapo, wamiliki wote wa ardhi nchini wamekumbushwa kuzingatia matumizi yaliyoainishwa kwenye hati miliki zao.
“Endapo mmiliki ana mpango wa kuendeleza ardhi kwa matumizi tofauti na yaliyoainishwa, anapaswa kupata kibali cha mabadiliko ya matumizi kama sheria zinavyoelekeza. Hii inalenga kuondoa migongano ya matumizi, kulinda mazingira na kudumisha mipango ya miji,” amesema Dk Akwilapo.
Amesisitiza kuwa uendelezaji wa ardhi lazima uzingatie Sheria za Mipango Miji, ikiwamo kupata vibali vyote kutoka mamlaka husika.
Ameongeza kuwa wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Tamisemi tayari wametumwa mkoani Geita kufuatilia mgogoro huo, huku Serikali ikiahidi kutoa taarifa rasmi baada ya uchunguzi kukamilika.
Januari 24, 2026, Waziri wa Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe, alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella, kufuatilia sakata hilo na kutoa mrejesho ndani ya siku 14, akisisitiza kuwa Serikali haiwezi kuchezewe hata na mtu mwenye fedha.
Mgogoro huo ulizuka baada ya kusambaa kwa video mitandaoni ikimuonesha Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma, akibishana na mwekezaji Rashid Kwanzibwa, akimtuhumu kubomoa nyumba nne za Serikali bila kibali katika eneo la Katoro Center. Baadhi ya majengo hayo yaliharibiwa wakati wa vurugu za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Kamati ya Fedha na Uchumi ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita, ikiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Jumanne Misungwi, ilitembelea eneo hilo na kubaini kuwa majengo yalibomolewa bila kibali cha Halmashauri, hivyo kumsimamisha mwekezaji huyo kuendelea na shughuli hadi suala hilo litakapopatiwa ufumbuzi.
Akieleza chanzo cha mgogoro, Mbunge Msukuma alisema kuwa baada ya ofisi za serikali kuchomwa moto wakati wa vurugu za uchaguzi, mwekezaji huyo alianza kusafisha eneo hilo bila kushirikisha Serikali, akidai kuwa alishirikiana na Mwenyekiti wa CCM wa kata husika.
Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi, Kwanzibwa alikanusha madai hayo akisema eneo hilo linamilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) na aliingia makubaliano rasmi na chama hicho kuanzia ngazi ya tawi.
Amesema baada ya kuanza kusafisha eneo hilo, alifika Mbunge Musukuma pamoja na Mbunge wa Katoro, Kija Ntemi, wakiwa na Kamati ya Fedha na Uchumi ya Halmashauri na kuanza kumuhoji kuhusu uhalali wa uwepo wake.
Kwanzibwa pia alidai kupigwa wakati wa tukio hilo, madai aliyoyaripoti Polisi Katoro na kupewa fomu ya matibabu (PF3). Kuhusu kubomoa majengo ya Serikali, amesema yalikuwa tayari magofu na hatarishi baada ya vurugu za uchaguzi, na alitoa taarifa kwa viongozi wa eneo hilo.
Kwa sasa, amesema anasubiri maamuzi ya CCM, akisisitiza kuwa bado hajaanza ujenzi bali amesafisha tu eneo husika.
