Ilichokisema Serikali shauri la Mwambe, familia yake kunyang’anywa pasipoti

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imekamilisha usikilizwaji wa shauri la maombi lililofunguliwa na Waziri wa zamani, Geofrey Mwambe, kupinga kunyang’anywa pasipoti zake mbili pamoja na za mkewe na watoto wao watatu, na imepanga kutoa uamuzi Januari 30, 2026.

Mwambe, ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mbunge wa Masasi (CCM), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji na Waziri wa Viwanda na Biashara, anadai pasipoti zake na za familia yake zilinyang’anywa na maofisa wa uhamiaji walipokuwa safarini.

Kutokana na tukio hilo, Mwambe kupitia mawakili wake, Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu, amefungua shauri la maombi ya dharura katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam dhidi ya Kamishna Mkuu wa Uhamiaji na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Katika maombi hayo anaomba mahakama imruhusu kufungua shauri la mapitio ya kimahakama ili Kamishna wa Uhamiaji aagizwe kuachia na kukabidhi pasipoti hizo.

Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo leo Jumatatu, Januari 26, 2026, Wakili Mpoki aliiambia mahakama kuwa hadi wakati huo wajibu maombi hawakuwa wamewasilisha kiapo kinzani, hali aliyodai inaonesha kuwa madai ya Mwambe hayajapingwa. Alisema kutokana na hali hiyo walijielekeza zaidi katika hoja za kisheria badala ya kiushahidi.

Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Vivian Method, alikiri kuwa hawakuwasilisha kiapo kinzani, akieleza kuwa Serikali ilikuwa imejipanga kujibu hoja za kisheria pekee, hususan suala la masilahi stahiki ya mwombaji katika shauri hilo.

Katika hoja zake, Wakili Mpoki alieleza kuwa katika hatua ya kuomba kibali cha kufungua shauri la mapitio ya kimahakama, mahakama inapaswa kuzingatia vigezo vitatu vya kisheria ambavyo ni kama kuna hoja inayobishaniwa, kama maombi yamefunguliwa ndani ya muda wa kisheria wa miezi sita na kama mwombaji ana masilahi stahiki katika suala linalobishaniwa.

Alisema hakuna ubishi kuwa kuna hoja inayobishaniwa na kwamba maombi yamefunguliwa ndani ya muda unaotakiwa kisheria, jambo ambalo hata wajibu maombi walilikiri, huku akisisitiza kuwa kigezo pekee kilichobaki ni suala la masilahi stahiki.

Akizungumzia kigezo hicho, Wakili Mpoki alidai kuwa Mwambe ana masilahi stahiki juu ya pasipoti zake na za familia yake kwa kuwa ndizo zinamzuia kusafiri, ikiwemo safari yake ya matibabu. Alieleza kuwa mke wake alipaswa kumsindikiza katika matibabu hayo na watoto wao wana haki ya kumiliki pasipoti zao isipokuwa kama wamefanya makosa chini ya Sheria ya Uhamiaji au Sheria ya Pasipoti na Hati za Kusafiria Tanzania.

Alisisitiza kuwa hakuna kosa lililofanywa na Mwambe wala familia yake linalohalalisha pasipoti zao kushikiliwa, akidai kuwa kitendo hicho ni ukiukwaji wa haki ya kikatiba ya uhuru wa kusafiri.

Kwa upande wake, Wakili Method aliomba maombi hayo yatupiliwe mbali akidai mwombaji hana masilahi stahiki ya kuomba pasipoti kwa niaba ya mkewe na watoto wake. Alieleza kuwa chini ya Kanuni ya 4 ya Kanuni za Marekebisho ya Sheria (Utaratibu wa Mapitio ya Kimahakama), ni mtu mwenye masilahi stahiki pekee anayeruhusiwa kufungua maombi ya kibali.

Alidai kuwa pasipoti ni hati binafsi kwa mujibu wa Sheria ya Pasipoti na Nyaraka za Kusafiria Tanzania, Sura ya 42, hivyo Mwambe hawezi kuomba kwa niaba ya watu wengine ambao si waombaji katika shauri hilo. Aliongeza kuwa kuna utaratibu wa kisheria wa kufungua mashauri kwa niaba ya watoto wadogo ambao haukuzingatiwa.

Akijibu hoja hizo, Wakili Mpoki alidai kuwa katika mashauri ya mapitio ya kimahakama suala linalozungumziwa  (locus standi) halitumiki kama ilivyo katika mashauri ya madai ya kawaida, akisisitiza kuwa kinachotakiwa ni kuonesha masilahi stahiki, ambayo alisema Mwambe anayo.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Ngunyale ameahirisha shauri hilo hadi Januari 30, 2026 kwa ajili ya uamuzi.