Dar es Salaam. Pea mbili za watoto pacha walioungana, Lightness na Loveness Luhende (1/5) pamoja na Nancy na Nice Sospeter (1/4), wameondoka kuelekea nchini Saudi Arabia kwa ajili ya matibabu ya kutenganishwa.
Pacha hao wanapelekwa leo Jumatatu, Januari 26, 2026 kwa matibabu hayo, baada ya kuwa chini ya uangalizi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja.
Kwa namna watoto hao walivyoungana, imeelezwa watahitaji matibabu yenye teknolojia ya hali ya juu pamoja na mabingwa wa upasuaji waliobobea.
Hayo amesema daktari bingwa mbobezi wa upasuaji watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Zaituni Bokhari wakati wa kuwaaga watoto hao katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere.
“Nancy na Nice Sospeter walizaliwa Agosti 30 mwaka 2024 Bunda mkoani Mara. Watoto hawa sasa wana mwaka mmoja na miezi mitano, wao wameungana kwenye tumbo, mpaka kwenye nyonga, wana miguu mitatu na wanashirikiana pamoja njia ya haja kubwa,” amesema.
“Lightness na Loveness Luhende walizaliwa Julai 30, 2024 wana mwaka mmoja na miezi minne. Wao wameungana kuanzia chini ya uti wa mgongo mpaka kwenye nyonga, wana miguu minne na kila mtoto ana njia yake ya haja kubwa na ndogo tofauti wao wanahitaji utaalamu wa hali ya juu kuweza kuwatenganisha.”
Dk Zaituni ambaye ameambatana na watoto hao kwenda kwenye matibabu Saudia, amekuwa karibu nao kwa kipindi chote walichokuwa Muhimbili.
Mama wa Nancy na Nice, Angelina George (38) kutoka Bunda Mara amesema alifikishwa Muhimbili Agosti 13 mwaka 2024 na wakati wote wamepokea huduma hospitalini hapo kwa gharama za Serikali.
“Nashukuru mkurugenzi wetu wa Muhimbili na Rais Samia Suluhu Hassan kwa msaada mkubwa aliotupatia tulipokuwa Muhimbili,” amesema Angelina akiongeza kuwa pacha hao ni uzazi wake wa saba.
Mama wa Lightness na Loveness, Mwalu Kilala (27) kutoka Itigi, mkoani Singida amesema watoto wake wana mwaka mmoja na miezi minne, huku akishukuru uongozi wa Muhimbili, Serikali na Falme ya Saudia kwa msaada.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Said Shaib Mussa ametoa shukurani kwa waziri wa Saudi Arabia kwa mashirikiano makubwa wanayoendelea kuboreshwa ndani ya miaka 50 katika mahusiano ya kidiplomasia.
Amesema tangu mwaka 2019 wa Saudi Arabia walisaidia tiba mbalimbali za utenganisho.
“Tumefanya ushirikiano mwingi katika tiba zipatazo 500 kupitia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete wenye thamani ya bilioni 4.5 zikihusisha upasuaji na utoaji wa vifaa mbalimbali,” amesema na kuongeza kuwa mashirikiano mengine yanayofanyika ni pamoja na kusomesha wataalamu.
Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk John Jingu ametoa shukrani kwa nchi ya Saudi Arabia, kwa kuwa si mara ya kwanza nchi hiyo kutoa msaada ya kutenganisha watoto walioungana kutoka Tanzania.
“Muhimbili wana uwezo wa kuwatenganisha pacha walioungana na walishawahi kufanya hivyo, lakini kazi hii inahitaji teknolojia na utaalamu wa juu, si hivyo tu lakini pia ni gharama sana kuwashughulikia.
“Udugu wa nchi zetu mbili unabeba hili jukumu, nitoe ombi balozi angalieni namna ya kuja kuwekeza katika jambo hili hapa nchini kwetu, kuna changamoto kama hizi nchi zinazotuzunguka, mkileta huduma kama hii basi itakua msaada kwa kiwango kikubwa sana,” amesema Dk Jingu.
Pia, amewapongeza Muhimbili kwa kuwatunza watoto hao mpaka kufikia umri wa mwaka mmoja na miezi kwa kuwahudumia na mpaka leo wanakwenda kutenganishwa, “Walipata huduma, kulelewa na hii sababu ina mchanganyiko mkubwa inabidi wapelekwe nje kwenye matibabu zaidi.”
Balozi wa Falme ya Saudi Arabia nchini Tanzania, Yahya bin Ahmed Okeish, ametoa shukrani zake kwa Dk Zaitun Bokhari kwa kazi yake kubwa anayoifanya katika kuhudumia watoto na timu nzima inayofanya kazi na daktari huyo, ambao huchakata kila kitu na kutoa huduma kabla ya upasuaji na baada.
Amesema programu hiyo ya upasuaji wa kutenganisha mapacha walioungana ni muhimu sana kwa Saudia na duniani kwa jumla na huja kwa maelekezo ya mfalme Suleiman.
Pia, amesema hutekelezwa kwa msaada mkubwa na ufuatiliaji wa mtoto wa mfalme na kusimamiwa na Dk Abdalah, na katika nchi zinazoneemeka na programu hiyo ni Tanzania.
“Hii ni programu inayokusanya wataalamu wabobezi na imeanza tangu mwaka 1990 ikiwa imebeba msaada wa kibinadamu na imefanya kazi ya kuwatenganisha watoto pea 60 ambazo zote zimefanikiwa na oparesheni moja hugharimu zaidi ya Dola za Marekani 100,000,” amesema.