Unguja. Wataalamu wa masuala ya bahari kutoka Tanzania, Kenya na Mauritius wamekutana Zanzibar kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto ya uvuvi haramu, wakisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda badala ya kila nchi kufanya jitihada zake kivyake.
Mkutano huo wa siku tatu unaofanyika Unguja umewakutanisha wataalamu wa bahari, watunga sera na wadau wa sekta ya uvuvi kutoka mataifa hayo matatu, ukiwa na lengo la kuimarisha usimamizi wa rasilimali za bahari na kudhibiti vitendo vya uvuvi haramu vinavyoathiri uchumi na mazingira.
Akifungua mkutano huo leo Januari 26, 2026, Naibu Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Mboja Khamis Mshenga, amesema Serikali inaukataa vikali uvuvi haramu kutokana na kusababisha madhara kwa rasilimali za bahari na mazalia ya viumbe wa majini.
“Tumezikaribisha hapa nchi ambazo tunazungukwa na bahari ili tuwe na mipango ya pamoja ya kukabiliana na changamoto hii. Uvuvi haramu unaharibu rasilimali zetu na kutishia mustakabali wa uchumi wa buluu,” amesema.
Amesema kuwa mapambano dhidi ya uvuvi haramu yanahitaji mshikamano wa kikanda, kwani bahari haina mipaka ya kijiografia, hivyo vitendo vinavyofanywa upande mmoja vinaweza kuathiri nchi jirani.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Hamad Khamis Hamad, amesema mkutano huo ni fursa ya kuzungumza kwa sauti moja ili maamuzi na sera zitakazokubaliwa ziweze kutekelezwa kwa ufanisi.
“Tukiharibu mazalia ya samaki, tunajiweka katika hatari kubwa kwa sababu bahari ndiyo tegemeo letu kuu. Ndiyo maana tunapaza sauti ya pamoja ili tulichokubaliana kisera kitekelezwe,” amesema.
Amesema Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2010 inatambua vitendo hivyo kuwa ni makosa, lakini Serikali ipo katika mchakato wa kuifanyia marekebisho ili iwe na nguvu zaidi katika kudhibiti uvuvi haramu.
“Sheria mpya itakuwa na maeneo ya uhifadhi yenye meno zaidi kuliko ilivyo sasa. Lengo ni kuhakikisha tunapambana kikamilifu na uvuvi haramu,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali imeweka mkazo zaidi kwenye elimu kwa wananchi badala ya kutumia nguvu, akisema katika maeneo yenye ushirikishwaji mkubwa wa jamii, uvuvi haramu umepungua kwa kiasi kikubwa. Sekta ya uvuvi, amesema, inasaidia zaidi ya watu 70,000 kulingana na mahitaji ya jamii.
Mwakilishi kutoka Kenya, Dk Paul Orine, amesema mafanikio ya mapambano dhidi ya uvuvi haramu yatapatikana endapo nchi zitatekeleza kwa vitendo makubaliano ya kikanda badala ya kila taifa kuwa na mpango wake tofauti.
Ameongeza kuwa bahari ni chanzo muhimu cha kipato kwa wananchi wengi katika nchi hizo, hivyo ulinzi wa rasilimali zake ni suala la moja kwa moja la maisha na ustawi wa watu.
Akizungumza kwa niaba ya Mradi wa Jahazi, msemaji wake Michael Mallya amesema lengo la mkutano huo ni kuzikutanisha serikali za ukanda wa Bahari ya Hindi zinazoshirikiana katika masuala ya bahari.
“Bahari ina mipaka ya kisheria, lakini kijiografia haina mipaka. Ndiyo maana ushirikiano ni muhimu, kwani kama hakuna udhibiti wa pamoja, meli kubwa zinaweza kuendelea kuharibu rasilimali zetu,” amesema.
Ameongeza kuwa uvuvi haramu unatishia pia sekta ya utalii na mapato ya wananchi, hivyo juhudi za pamoja ni muhimu ili kulinda uchumi wa nchi za ukanda huo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Uhifadhi wa Bahari, Mohamed Soud Mohamed, amesema uvuvi haramu umekuwa na athari kubwa kiuchumi, kimazingira na kiikolojia.
Amesema kupitia mkutano huo, nchi za Afrika Mashariki na Kati zitaweka mipango jumuishi ya kukabiliana na changamoto hiyo ili kulinda rasilimali za bahari kwa kizazi cha sasa na kijacho.
