Katakata CCM yashika kasi, yaibua mjadala

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa muda mrefu kimekuwa kikitekeleza utaratibu wa uteuzi wa wagombea wa ubunge na nafasi nyingine za uwakilishi kupitia kura za maoni, ambao mwisho wa mchakato huibua mjadala ndani na nje ya chama.

Hali hiyo, iliyoainishwa wazi katika Katiba ya CCM, imejenga mjadala mpana kuhusu mizani kati ya demokrasia ya ndani ya chama, ikiangazia mamlaka ya wajumbe kupata viongozi wanaowataka, na uongozi wa juu unaolenga kulinda maslahi mapana ya chama kwa viongozi wake.

Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, kura za maoni zinazopigwa na wajumbe katika ngazi za chini huwa ni ushauri au mapendekezo tu, huku uamuzi wa mwisho wa nani ateuliwe kugombea nafasi za udiwani, ubunge au nyingine za uwakilishi hutolewa na vikao vya juu, Kamati Kuu au Halmashauri Kuu.

Katika mtazamo huo, kura za maoni peke yake haziwezi kuwa kigezo cha mwisho, hasa pale zinapodaiwa kuathiriwa na makundi, fedha au hisia za muda. Hata hivyo, kwa ngazi ya wajumbe na jamii kwa ujumla, utaratibu huo umekuwa ukiibua hisia tofauti.

Tukio la karibuni ni la Jimbo la Peramiho, Mkoa wa Ruvuma, ambapo aliyeongoza kura za maoni, Victor Mhagama, amewekwa kando na Kamati Kuu ikamteua aliyeshika nafasi ya tano, Dk Lazaro Komba, kuwania ubunge katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Februari 26, 2026.

Katika uchaguzi mkuu wa 2025, wa mwaka 2015 na hata 2010, baadhi ya walioongoza kura za maoni ndani ya chama walijikuta wakifyekwa na kuteuliwa walioshika nafasi ya pili, tatu, nne au tano. Mijadala iliibuka na baadhi waliamua kuhama vyama.

Miongoni mwa walioongoza kura za maoni mwaka 2025 za ubunge na kujikuta wakiwekwa kando na kuteuliwa wengine katika majimbo yao ni Ummy Mwalimu (Tanga Mjini), Fredrick Lowassa (Monduli), Priscus Tarimo (Moshi Mjini), Kilumbe Ng’enda (Kigoma Mjini), Michael Kembaki (Tarime Mjini) na Robert Maboto (Bunda Mjini).

Akizungumzia suala hilo na kinachofanyika kwenye uteuzi wa mwisho, mmoja wa viongozi waandamizi wa CCM aliyeomba hifadhi ya jina lake, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu, amesema chama kinaheshimu maoni na uamuzi wa vikao vyake vya ngazi zote ili kufanya uamuzi sahihi.

Amesema mafanikio ya chama hicho, ambacho kimeendelea kubaki madarakani kwa miongo zaidi ya sita, kimefika hapo kutokana na kuheshimu maoni na sauti za wananchi.

“Wanaosema chama hakiheshimu maoni ya wajumbe hawana hoja za msingi. Chama hiki kimefika hapa kwa kuheshimu sauti za wananchi,” amesema kiongozi huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake.

Ameweka wazi kuwa yule anayechaguliwa na wajumbe kwenye vikao vya chini ndiye hupewa nafasi na vikao vya juu, isipokuwa kama kuna tuhuma za mambo mengine dhidi yake.

“Huyo anayechaguliwa na wajumbe kwenye vikao halali ndiye huyo huyo huteuliwa, vinginevyo kama kuna mambo mengine,” amesema.

Baadhi ya wajumbe wanaona hatua hiyo ni mfumo sahihi unaolinda chama dhidi ya migawanyiko na viongozi kupita kwa rushwa ngazi za chini. Kwao, vikao vya juu vina taarifa pana zaidi kuhusu mgombea, historia yake ndani ya chama na athari za uteuzi wake kwa taswira ya CCM kitaifa.

Mmoja wa wajumbe wa CCM Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam (jina limehifadhiwa) ameliambia Mwananchi kuwa vikao vya juu vinafanya hivyo kwa kuzingatia maslahi ya chama.

“Viongozi wa juu wanaangalia mambo mengi, ikiwemo mwelekeo wa Serikali, kwa hiyo lazima wachuje upya maana huku chini mtu anaweza akapitishwa tu hata kwa kujuana,” amesema, akionesha kuunga mkono mtazamo kwamba uamuzi wa juu ni kichujio cha mwisho cha kulinda maslahi ya chama kwa ujumla.

Kwa upande mwingine, kuna wajumbe na wanachama wanaodai utaratibu huo unadhoofisha dhana ya demokrasia ya ndani ya chama na uwakilishi wa wananchi.

Mjadala huo umeonekana zaidi katika ngazi za ubunge na kushuka hadi udiwani, ambako wajumbe wa matawi na kata huhusika moja kwa moja katika kura za maoni.

Baadhi ya maeneo, uteuzi unaobadilisha matokeo ya kura za maoni umekuwa ukiibua migawanyiko, ikiwemo baadhi ya makada wanaokatwa majina yao kukihama chama, wengine kuibua migogoro ndani ya chama, huku wanaoonekana kuwa kinyume na walioteuliwa wakipewa jukumu la kuongoza kampeni za maeneo hayo ili kuficha hisia zao mbele ya umma.

Baadhi ya wajumbe kutoka ndani ya chama wanasema ingawa Katiba ya CCM inatoa mamlaka hayo kwa vikao vya juu, changamoto imekuwa namna mamlaka hayo yanavyotekelezwa na kueleweka kwa wanachama wa kawaida, hali wanayosema imekuwa ikiwagawa wanachama hasa pale mtu anayependwa sana anapokatwa jina lake na vikao vya juu.

“Kwa kweli hali hii imekuwa mbaya mno, yaani sisi tunachagua mtu tunayemtaka, halafu huko juu wanamkata na tunaletewa mtu mwingine. Sisi kwenye uchaguzi wa 2025 tuliletewa mtu ambaye hata hatumfahamu, tukaambiwa huyu ndiye anatakiwa. Basi kwa kuwa mwana CCM unatakiwa usimame na CCM, tulisimama naye na akashinda,” amesema mjumbe mwingine kutoka Temeke, Dar es Salaam.

Ameongeza kuwa mchakato wa uteuzi unaofanywa na ngazi za chini unapotenguliwa na vikao vya juu husababisha mipasuko ndani ya chama, ikiwemo baadhi ya wanachama kukihama chama hicho na wengine kususia mchakato wa uchaguzi.

Hata hivyo, ni muhimu pia kutambua kuwa suala hili si jipya, limekuwepo kwa muda mrefu na limejadiliwa katika vipindi tofauti vya uchaguzi za CCM, lakini kila awamu huibua upya mjadala uleule: je, CCM ibaki na mfumo wake wa sasa unaotoa uzito kwa uamuzi wa juu, au iboreshe namna kura za maoni zinavyotumika ili kuongeza imani ya wajumbe?

Kwa mtazamo wa kitaasisi, CCM inaendelea kusisitiza kuwa nguvu ya chama chake iko kwenye umoja na nidhamu. Ndiyo maana Katiba yake imejenga mfumo unaoweka uamuzi wa mwisho juu, ili kuzuia migawanyiko inayoweza kukigharimu chama kisiasa.

Hata hivyo, kwa upande wa wanachama, swali linaloendelea kuulizwa ni kama kulinda mshikamano wa chama kunapaswa kwenda sambamba na kuimarisha zaidi sauti ya wajumbe, huku wachambuzi wa siasa wakitaja mwenendo huo wa CCM kama kikwazo kwa ustawi wake na demokrasia ya wananchi.

Mmoja wa wabunge waliogombea nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, ambaye jina lake halikupendekezwa, amesema uamuzi wa chama lazima uheshimiwe licha ya ukweli kwamba walipaswa kuweka uwanja huru ili kila mtu ajipime kukubalika kwake kwa wabunge.

Mbunge huyo amekiri kuwa uamuzi wa CCM kwa sasa ni wa upepo, na wanakwenda namna unavyovuma, hivyo haitakiwi kulalamika bali kusubiri wakati mwingine.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Dk Richard Mbunda, amesema mfumo wowote wa kisiasa unapaswa kujengeka kwenye mamlaka halali, aidha kwa kusomea au kuchaguliwa na wananchi.

Amesema kinachofanyika ndani ya CCM kinapoka haki ya wananchi kupata viongozi wanaowataka katika maeneo yao.

“Mchakato wa kisiasa unataka yule anayechaguliwa huko ngazi za chini ndiye anaonekana kupendwa na kuhitajiwa na wananchi. Hii ya kuchaguliwa na wengi, baadaye kamati inakaa na kuamua tu kata huyu peleka yule, inaathiri chama hicho na kutengeneza mpasuko,” amesema na kuongeza:

“Mimi ningetamani kuona CCM inazingatia kura za wajumbe isipokuwa kama huyo aliyechaguliwa ana matatizo makubwa ya kimaadili au kinidhamu, vinginevyo chama kinajitengenezea bomu kwa kujenga imani kuwa kura za wajumbe haziamui chochote ndani ya mchakato wa kupata wagombea,” amesema.

Mchambuzi mwingine wa masuala ya siasa nchini, Wakili Aloyce Komba, amesema kwa CCM kukata majina ya wagombea ngazi za juu ni utekelezaji wa kanuni zake halali, akisema hatua hiyo inafanya maoni ya wanachama kuwa si uamuzi wa mwisho kisheria ndani ya chama hicho.

“Wagombea waliokubaliwa kwa kura za maoni wakienguliwa, wengine huhama chama, huunda makundi, hupiga kura za maruhani, pia baadhi ya wanachama huhisi demokrasia inaminywa, huku Kamati Kuu ikionesha nguvu zake kuwa inalinda nidhamu ya chama,” amesema.

Wakili Komba amesema ili kuondoa hali hiyo kwenye mifumo ya vyama vya siasa, suluhisho ni kupigania ugombea binafsi ili kutoa nafasi kwa wanaotaka uongozi bila chama kuwa na haki kikatiba.

“Kuondokana na vikwazo hivi kwenye siasa zetu, takwa la kuwa na mgombea binafsi kama alivyopigania marehemu Mchungaji Christopher Mtikila linapaswa kupewa kipaumbele ili kupanua demokrasia, uwajibikaji, na uchaguzi huru nchini kwa mustakabali wa siasa jumuishi,” amesema.